WALIMU HAWANA OFISI,WAFANYA KAZI CHINI YA MKOROSHO,WANAFUNZI NAO WAJISAIDIA VICHAKANI

 
SHULE ya Msingi Vikawe iliyopo Kata ya Pangani wilayani Kibaha mkoani Pwani inakabiliwa na changamoto ukiwemo upungufu wa matundu ya vyoo, madarasa na ofisi ya walimu na hivyo kufanya shule kutokuwa na mazingira rafiki ya utoleaji elimu.

Aidha wanafunzi wengi wanalazimika kujisaidia vichakani kutokana na upungufu wa matundu.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Albert Nsajigwa amesema hata walimu hufanya kazi zao wakiwa chini ya mti.

Nsajigwa amesema walimu hao wamekuwa wakifanya majukumu yao chini ya mkorosho na kujiuliza hali inakuwaje inaponyesha mvua ilihali shule hiyo ikiwa na madarasa saba na kati ya hayo mawili yanatakiwa kuvunjwa kutokana na uchakavu.

"Tunaomba wadau watusaidie kwani hali ni mbaya sana miundombinu si rafiki kwa wanafunzi hata walimu na tulipeleka maombi yetu halmashauri kwa ajili ya kutusaidia lakini inaonekana mambo hayajawa mazuri na tukaona bora tuanze ujenzi wa vyoo vinne kwa nguvu ya wananchi," amesema Nsajigwa.

Amesema kutokana na uhaba wa madarasa wanafunzi wa awali maarufu kama chekechea wanasomea nje hivyo kuna haja ya wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia.

Diwani wa Kata ya Pangani, Augustino Mdachi amesema shule hiyo kongwe kabisa katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombinu na hivyo kuathiri suala zima la utoaji na upataji wa elimu shuleni hapo.

Mdachi amesema katika mwaka wa fedha 2O16 /2017 Halmashauri ya Mji wa Kibaha katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo kama ilivyoainishwa katika taarifa yake, imetenga jumla ya Sh milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za Kambarage, Vikawe, Maendeleo, Mkoani, Mwanalugali, Sofu na Lumumba.

Amesema kwa upande wa vyumba vya madarasa jumla ya Sh milioni 54, kwa shule za msingi Mamlaka, chumba kimoja cha darasa na Vikawe vyumba viwili vya madarasa na hiyo inategemea makusanyo ya ndani ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
 Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post