Picha: WAATHIRIKA WA NDOA ZA UTOTONI WALILIA KUBADILISHWA SHERIA YA NDOA,AGAPE AIDS CONTROL PROGRAMME, MSICHANA INITIATIVE WAUNGANA


Katikati ni Muathirika wa ndoa za utotoni Pili Omary akizungumza na waandishi wa habari leo katika kituo cha kujiendeleza kielimu kwa wahanga wa mimba na ndoa za utotoni kilichopo mjini Shinyanga kinachoendeshwa na Shirika la Agape Aids Control Programme linalohusika na utetezi wa haki za watoto.Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde,anaripoti.


Akizungumza katika kikao hicho kilichoandaliwa na shirika la Agape Aids Control Programme na Msichana Iniatiative Omary ameiomba serikali kupitia wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto na wizara ya Katiba na Sheria na taasisi mbalimbali kuongeza kasi katika jitihada za kubadili vifungu vya sheria ya ndoa ya namba 5 ya mwaka 1971.

Vifungu hivyo vya sheria vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na miaka 15 kwa ridhaa ya mahakama.

“Kupitia shirika la Agape Aids Control Programme na Msichana Initiative yanayolea watoto walioathirika na ndoa za utotoni,tunaomba wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto na wizara ya Katiba na Sheria,bunge na mwanasheria mkuu pamoja na taasisi mbalimbali kuongeza jitihada za kuibadili sheria hii na sheria nyingine kinzani zinazomkandamiza mtoto wa kike katika kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu”,alieleza Omary.

*********
IFUATAYO NI TAARIFA YA SHIRIKA LA AGAPE AIDS CONTROL PROGRAMME NA MSICHANA INITIATIVE KUHUSU NDOA ZA UTOTONI ILIYOSOMWA NA MUATHIRIKA WA NDOA ZA UTOTONI PILI OMARY 





Ndoa za Utotoni Zinakwamisha Maendeleo ya Mtoto wa Kike, Umri wa Kuolewa Uanzie Miaka 18.

Ndugu wanahabari,
Awali ya yote tungependa kuwashukuru kwa kujiunga nasi siku hii ya leo. Tunatambua na kuheshimu mchango wa vyombo vya habari katika kuchochea mabadiliko chanya kwenye jamii yetu.

Pia tungependa kuchukua fursa hii kutambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali katika kuleta ustawi na maendeleo ya watoto hasa mtoto wa kike.

·        Serikali kupitia wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatambua na imekuwa mstari wa mbele kuzungumzia tatizo la ndoa na mimba za utotoni. Kwa kuthibitisha hilo, mwaka huu imeadhimisha siku ya “Mtoto wa kike duniani” yenye kauli mbiu isemayo “Mimba na Ndoa za Utotoni zinaepukika, chukua hatua Kumlinda Mtoto wa Kike” ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 11 ya mwezi Octoba iliyofanyika kitaifa mkoani Shinyanga ili kutia hamasa kwa jamii kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na Mimba za utotoni.

·        Kupitia taasisi na idara za serikali tumeona ufanisi na juhudi mbalimbali za kimakusudi zikichuliwa katika kulinda na kutetea haki ya mtoto wa kike.

·        Wadau mbalimbali ikiwemo Mashirika yasiyo ya kiserikali, Mashirika ya dini na Washirika wa Maendeleo wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali kufikia malengo ya kitaifa ya kulinda na kutetea haki za Mtoto wa Kike; hii ni kulingana na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayohusu ustawi na maendeleo ya mtoto wa Kike ambayo Tanzania imeridhia.

Pamoja na jitihada kubwa ambazo serikali na wadau mbalimbali wanafanya bado kuna changamoto katika kutatua na kumaliza kabisa tatizo la ndoa za utotoni katika Taifa letu.

Hali ya Ndoa za Utotoni Ikoje Tanzania?

Takwimu za ndoa za utotoni duniani zinaonesha kuwa, Tanzania ni moja ya nchi zenye viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni. Aidha Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti wake uliochapishwa mnamo Januari,2016 uliitaja Tanzania kuwa nchi ya tatu (3) katika bara la Afrika kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni kwa asilimia 28. 

Kutokana na shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), kwa wastani watoto wakike wawili (2) kati ya watano (5) huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Kutokana na takwimu za utafiti wa Idadi ya watu na Afya Tanzania (TDHS, 2010) asilimia 37% ya watoto wa kike Tanzania huolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Kutokana na takwimu za shirika la Watoto Duniani (Unicef 2012) kitaifa mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa matukio ya ndoa za utotoni (59%), ukifuatiwa na Tabora (58%), Mara (55%), Dodoma (51%), Lindi (48%), Mbeya (45%), Morogoro (42%), Singida (42%), Rukwa (40%), Ruvuma (39%), Mwanza (37%), Kagera (36%), Mtwara (35%), Manyara (34%), Pwani (33%), Tanga (29%), Arusha (27%), Kilimanjaro (27%), Kigoma (26%), Dar es Salaam (19%) na Iringa (8%).

Hata hivyo, tatizo hili linachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo:

1.   Mila na desturi potofu
2.   Sheria na sera kinzani
3.   Mifumo dhaifu ya uongozi katika ngazi ya kata, vijiji, Mitaa na vitongoji

Athari za Ndoa za Utotoni
Ndoa za utotoni ni suala la kiafya, kielimu na kisaikolojia.

·     ➤Mtoto wa kike anayeolewa katika umri mdogo ananyimwa fursa ya kujiendeleza kielimu na kumaliza masomo na hatimaye kufikia ndoto zake za maisha.
      ➤Msichana kujifungua katika umri mdogo ni chanzo cha matatizo kama fistula na vifo vingi vya wajawazito.
        ➤Maambukizi ya magonjwa ya zinaa na VVU/UKIMWI
   Mtoto anayeolewa katika umri mdogo anaathirika 
kisaikolojia kutokana na kupewa majukumu makubwa na kupitia mambo ambayo yako juu ya uwezo wake. Watoto wengi wanaoolewa wakiwa wadogo ni waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

   ➤Ndoa za utotoni zinazima nafasi ya watoto wa kike kuweza kujiendeleza na kuchangia katika uchumi wa jamii zao na taifa kwa ujumla, na hivyo kupelekea mzunguko wa umaskini kuendelea miongoni wa familia zao.

Ombi la shirika la Agape AIDS Control Programme na Msichana Initiative Kwa Serikali:

 (Bunge, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Katiba na Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali).

Shirika la Agape na Msichana, tunatambua jitihada zinazoendelezwa na serikali katika kubadili vifungu vya sheria ya ndoa No.5 ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na miaka 15 kwa ridhaa ya mahakama.

Kwa kuzingatia athari wanazozipata wasichana kutokana na tatizo hili, tunaiomba serikali kupitia wizara na taasisi husika kuongeza kasi kwenye jitihada za kuibadili sheria hii na sheria nyingine kinzani


zinazomkandamiza mtoto wa kike katika kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu.
Sisi kama wadau tunaotetea haki na usalama wa mtoto hasa wa kike, tuko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali yetu pindi muswada utakapokuwa tayari na kuhitaji maoni ya wadau ili kuwa na sheria bora na yenye nguvu, itakayolinda na kutetea maslahi mapana ya watoto wote wa Tanzania.

Hitimisho
Suala la ndoa za utotoni katika taifa letu linahitaji nguvu ya pamoja na ya kila mmoja wetu ili tuweze kulitokomeza. Kila mmoja wetu ana nafasi ya kuchangia kwenye jitihada za kumaliza tatizo hili kabisa. Tungependa kuomba ushirikiano kutoka kwa kila mmoja wetu, ili tuweze kujenga jamii yenye kulinda haki na kujenga ustawi imara wa watoto katika nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania;
Ahsanteni Kwa Kunisikiliza

Imesomwa Kwenu na:
Pili Omary - Muathirika wa Ndoa za Utotoni
Leo Tarehe: 23 Novemba 2016

Angalia matukio katika picha wakati wa kikao hicho 
Pichani kulia ni Kaimu mkurugenzi wa Shirika la Aids Control Programme linalohusika na utetezi wa haki za watoto,Samwel Magina,katikati ni muathirika wa ndoa za utotoni Pili Omary anayelelewa katika kituo hicho,wa kwanza kushoto ni mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative linalohusika na utetezi wa haki za watoto wa kike,Rebeca Gyumi.
Muathirika wa ndoa za utotoni Pili Omary(katikati) akielezea athari za ndoa za utotoni ambazo ni mtoto wa kike kunyimwa fursa ya kujiendelea kielimu,kupata matatizo ya fistula kutokana na kujifungua katika umri mdogo,kupata magonjwa ya zinaa na VVU/Ukimwi,kuathirika kisaikolojia kutokana na kupewa majukumu makubwa na kupitia mambo ambayo yako juu ya uwezo wake na kuzima nafasi ya watoto wa kike kujiendelea kiuchumi hivyo kusababisha umaskini katika familia zao.
Omary alisema tatizo la ndoa za utotoni linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi potofu,sheria na sera kinzani,mifumo dhaifu ya uongozi katika ngazi ya vijiji,mitaa na vitongoji
Katikati ni mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative linalohusika na utetezi wa haki za watoto wa kike,Rebeca Gyumi akizungumza katika kikao hicho ambapo alisema hivi sasa shirika lake limeungana na shirika la Agape Aids Control Programme la mjini Shinyanga katika kupiga vita mimba na ndoa za utotoni.Gyumi alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau mbalimbali wa haki za watoto kuungana pamoja katika kupiga vita suala la ndoa za utotoni
Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative,Rebeca Gyumi aliiomba serikali kuongeza nguvu katika kulinda na kutetea haki za mtoto wa kike kwa kubadilisha sheria zinazomkandamiza mtoto wa kike
Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative,Rebeca Gyumi akiwakabidhi watoto walioathirika na ndoa za utotoni tuzo "Global Goal Awards 2016" aliyopewa na Umoja wa mataifa kupitia mradi wa maendeleo endelevu ambapo mwaka huu Umoja wa Mataofawalijikita katika masuala ya wasichana na kutokana na shirika lake kuchukua hatua katika masuala ya wasichana ikiwemo jitihada zake katika kupinga ndoa za utotoni ndiyo maana akapewa tuzo hiyo kwa kufikia lengo hilo.
Januari mwaka huu Rebeca Gyumi alifungua kesi mahakama kuu kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayotoa mwanya kwa watoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 na mtoto wa kiume kuoa akiwa na umri wa miaka 18 akidai vifungu hivyo vinabagui watoto na Julai 08,2016 mahakama ilitoa uamuzi ukiwa wao hivyo kufanikiwa kushinda kesi hiyo na kusema kuwa vifungu hivyo viko kinyume na katiba,pia vinaminya ustawi wa jamii na umri wa chini sasa itakuwa miaka 18 kwa mtoto wa kike na kiume hivyo kinachotakiwa ni kubadili vifungu hivyo kupitia bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania
Kaimu mkurugenzi wa Shirika la Aids Control Programme linalohusika na utetezi wa haki za watoto,Samwel Sasaba Magina alisema kutokana na hamasa kuhusu madhara ya ndoa za utoto wanayoifanya kwa kushirikiana na wananchi na jeshi la polisi idadi ya watoto wa kike waliothirika na ndoa za utotoni imezidi kuongezeka katika kituo chao cha kulelea watoto hao.
Magina alisema Mei mwaka huu wahanga wa ndoa za utotoni walikuwa 57 lakini mpaka mwezi Novemba mwaka 2016 idadi imefikia 122 na wote wanalelewa katika kituo cha kujiendeleza kielimu kwa wahanga wa mimba na ndoa za utotoni kilichopo mjini Shinyanga lengo ni kuwafanya watoto hao watimize ndoto za kimaisha. 
Bango lililopo katika Kituo cha Kujiendeleza Kkielimu kwa wahanga wa ndoa na mimba za utotoni,vijana na jamii kwa ujumla na watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi kinachomilikiwa na Shirika la Agape Aids Control Programme (AACP)
Mwonekano wa jengo linalotumiwa na wahanga wa ndoa na mimba za utotoni-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post