MWENYEKITI ATAKA APIGWE RISASI MBELE YA MKUU WA MKOA

MWENYEKITI wa Soko la Mbande wilayani Temeke, Mukiwa Hassani ameomba kupigwa risasi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ikiwa itathibitika amekula fedha za vizimba katika soko hilo. 

Mwenyekiti huyo alifikia hatua hiyo, baada ya kutuhumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo mbele za Makonda kwamba amekuwa akikusanya kiasi cha Sh 400,000 za vizimba kinyume cha taratibu na kutoa risiti hewa. 

Makonda amemtaka Hassani ajibu tuhuma hizo mbele za wananchi na kueleza bayana alielekezwa na mamlaka gani kukusanya fedha hizo na akikusanya anazipeleka wapi. 

Hassani alikana tuhuma hizo na kudai kwamba walikubaliana na wafanyabiashara hao kabla ya ujenzi wa soko ambalo liko chini ya mwekezaji kuwa litakapokamilika wafanyabiashara wote watakaohitaji vizimba watalazimika kuchangia gharama za ujenzi. 

Amesema hakuna mfanyabiashara aliyetoa fedha na kumpatia na endapo atakuwa anaeleza uongo basi yuko radhi apigwe risasi na kufa mbele ya mkuu huyo. 

"Mkuu wa Mkoa, kama wanasema nimechukua fedha waseme walinipa lini na kama nilichukua fedha ya mtu yeyote, basi nipigwe risasi nife hapahapa,"amesema. 

Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara walimuunga mkono mwenyekiti huyo hali iliyoibua mkanganyiko uliomfanya Makonda kutoa maamuzi. 

"Naomba Mkuu wa Wilaya na wahusika mfutilie kujua mwekezaji wa soko, sababu ya fedha Shilingi 400,000 zinazokusaywa kwa ajili ya vizimba zinaelekezwa kwa nani na kwa maelekezo ya nani,"amesema Makonda. 

Makonda anaendelea na ziara ya siku 10 kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post