VYUO VIKUU 15 KITANZINI,CHANZO MATOKEO YA MITIHANIKatibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi
SERIKALI imetoa siku mbili kwa vyuo vikuu 15, kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ya wanafunzi wanufaika na mikopo wanaoendelea na masomo ili kupangiwa mikopo kwa mwaka wa 2016/2017.

Vyuo hivyo vilivyokuwa viwasilishe matokeo hayo siku 30 kabla ya kufunguliwa, vimepewa siku hizo kuanzia jana, kabla serikali haijachukua hatua zozote.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi alisema hayo jana, alipotembelea ofisi za Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Alisema serikali iko katika hatua za mwisho za upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo.

Tarishi alisema baadhi ya vyuo vimeshindwa kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wanaoendelea ili wapangiwe mikopo kwa mwaka unaoendelea, kwani utaratibu lazima vyuo kuwasilisha matokeo kuonesha wanafunzi wangapi wana sifa za kuendelea kupewa mikopo.

“Mikopo haiwezi kutolewa tu kwa kila mwanafunzi, hata kama ameamua kuacha masomo, hivyo vyuo vina wajibu wa kuthibitisha kuwa wanafunzi wanaowaleta bado ni wanafunzi sahihi na wanaendelea na masomo,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Alivitaja vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo hayo kuwa ni Vyuo vya Elimu ya Biashara (CBE) Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UOB), Chuo Kikuu cha St. John Kituo cha St Mark Dar es Salaam (SJUTDSM), Chuo cha St. John Tanzania (SJUT) na Chuo Kikuu cha Tumaini Mbeya (TUMAMBEYA).

Vingine ni Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI), Chuo cha United African University of Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph cha Tiba ya Sayansi (STJCAHS), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Kituo cha Makambako na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).

Katibu Mkuu huyo pia alitaka vyuo hivyo kuimarisha mifumo yao ya kuandaa na kuwasilisha matokeo ya mitihani kwa wakati na kwa ukamilifu katika siku zijazo ili kuondoa usumbufu. Akizungumzia hatua watakazochukua wasipotimiza agizo hilo, alisema wanawaagiza kutekeleza maagizo hayo kwa siku walizopewa.

Alisema ana uhakika kauli hiyo inawatosha waungwana hao, kutimiza wajibu wao.

Awali vyuo vyote vya elimu ya juu, vilikumbushwa umuhimu wa kuwasilisha matokeo, kabla havijafunguliwa, ikiwemo serikali kufanya mkutano na Makamu Wakuu wa vyuo vyote vya elimu ya juu mkoani Dodoma na kusisitiza umuhimu wa vyuo kuwasilisha matokeo na nyaraka nyingine muhimu, kabla ya vyuo kufunguliwa.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga kikamilifu na imetenga fedha za kutosha na tayari imetoa Sh bilioni 80.89 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, wanaonufaika na mikopo hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka.

Alisema kati ya kiasi hicho, tayari Sh bilioni 45.2 zimekwishalipwa na kiasi kilichosalia, kitalipwa kwa vyuo baada ya kupokea matokeo kikamilifu. Pia aliwatoa wasiwasi wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokosa mikopo, kupeleka malalamiko katika dirisha maalum la malalamiko, lililofunguliwa na Bodi ya Mikopo kuanzia juzi na serikali ni sikivu, itafanyia kazi.

Katika siku za hivi karibuni, wanafunzi wa elimu ya juu katika vyuo mbalimbali wanaoendelea na masomo, wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kwa mikopo ya elimu ya juu ; huku wanaoanza mwaka wa kwanza, wakilalamikia kukosa mikopo hiyo.

Imeelezwa kuwa baada ya kufanyika uchambuzi, wanafunzi 20,183 wanaoanza mwaka wa kwanza katika vyuo mbalimbali wamepatiwa mikopo; huku wakitarajia kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amesema serikali kwa sasa inaandaa taarifa kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na ikishakamilika itawasilisha bungeni, kama walivyoomba wabunge.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kujibu mwongozo uliotolewa na Mbunge wa Mwibara, Kange Lugola (CCM) kuomba mwongozo bungeni, akitaka leo serikali ilete taarifa kuhusu mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo, kwa kile alichoeleza kuwa wanafunzi wengi walioomba mikopo wakiwa na vigezo, hawajapata. Jenista alisema kwa sasa serikali inaandaa taarifa hiyo na ikikamilika, italetwa bungeni kama wabunge walivyoomba.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali pamoja na mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itadhibiti utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi waliokidhi vigezo pekee, ndio wananufaika kwa mikopo hiyo.

Awali, Mhagama alisema serikali haifanyi kazi kwa miujiza, bali kwa kutumia mgangilio wa bajeti iliyowekwa na uthibitisho kwamba serikali inafanya kazi kwa mipango, imeweza kutekeleza kutoa elimu bure ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mhagama alitoa kauli hiyo baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Free Mbowe (Chadema) kuuliza swali la nyongeza lililotokana na swali la msingi la Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele (CCM) kutaka kujua Serikali itaanza kutekeleza lini ahadi ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa ili kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na akina mama.

Akifafanua zaidi, alisema kamwe serikali haijiendeshi kwa miujiza bali kwa kutumia mipango iliyojiwekea katika bajeti zake.

“Kuthibitisha jambo hili linatekelezeka, Serikali ya CCM kupitia Ilani yake tumeweza kutoa elimu bure, kuwashangaza Watanzania miradi mikubwa mbalimbali imetekelezwa ikiwemo kununua ndege (mbili za Dash 8, Q400 zilizotengenezwa na Bombardier), Ilani inatekelezwa kwa mambo mengi mbalimbali,” alisema akimjibu swali la nyongeza Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) kuhusu Sh milioni 50 zilizoahidiwa kwa kila kijiji nchini.

Jenista alisema fedha zote zinazoahidiwa na serikali zikiwemo Sh milioni 50, zitatolewa na Watanzania watazipata.

Imeandikwa na Gloria Tesha, Dodoma na Theopista Nsanzugwanko, Dar wa gazeti la Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post