VYETI FEKI VYA VIFO VYA WAZAZI VYATUMIKA KUPATA MIKOPO ELIMU YA JUU TANZANIA

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imebaini kuwepo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane kama ni watoto yatima; hivyo wapewe kipaumbele cha kupatiwa mkopo.

Kuwepo kwa vyeti hivyo vya bandia kumegunduliwa na bodi hiyo baada ya kupeleka nakala za vyeti vyote vya vifo ofisi ya Msajili wa Vizazi na Vifo (Rita) kwa ajili ya uthibitisho ndipo ikagundulika kuwepo kwa kasoro hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, amesema  kuwa wahusika wote ambao wamewasilisha vyeti hivyo feki suala lao limekabidhiwa kwa mamlaka zinazoshughulika na makosa ya jinai.

Hata hivyo, Badru hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo kwa maelezo kuwa bado wanaendelea na ukaguzi.

“Bado tunaendelea kuchunguza na idadi yao hapa sina, tukikamilisha tutawaita kuwaambia idadi yao,” alisema Badru na kuongeza kuwa kutokana na kasoro hizo, ndio maana kuna baadhi ya watu wanaolalamika kuwa ni yatima, lakini hawakupata mkopo.

“Hayo malalamiko ya kwamba kuna yatima wamekosa mikopo tumeyasikia, lakini na sisi tunajiridhisha kuwa huyu ni yatima baada ya kupata uthibitisho wa vyeti vya vifo kutoka Rita,” alisema Badru.

Aliongeza kuwa hata wale ambao ni wanafunzi wenye ulemavu, bodi hiyo haiwezi kuwaamini kama ni walemavu, bali hadi wapate uthibitisho kutoka kwa daktari wa wilaya (DMO) kuthibitisha ulemavu wa mwombaji.

Alisema baadhi ya wanafunzi ambao wanalalamika kuwa wamekosa mikopo ni wale ambao maombi yao yalikaguliwa na kukutwa na dosari kadhaa, na wakaombwa wazirekebishe kasoro hizo, lakini baadhi yao hawakufanya hivyo.

Badru alisema bodi yake baada ya kuchambua maombi ya waombaji wote; hadi sasa imeshatoa mikopo kwa wanafunzi wote wanaostahili wakiwemo yatima, walemavu, wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele na wahitaji wanaosoma kozi zingine.

Akizungumzia suala la baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambao wamekosa mikopo na kulazimika kurudi makwao, Badru alisema wanafunzi hao yawezekana ni miongoni mwa wale ambao hawakukidhi vigezo vya kuweza kupewa mkopo.

“Pale Dodoma tumetoa mkopo kwa wanafunzi wapya takribani 3,000, hivyo hao wanaoondoka kurudi nyumbani yawezekana wako kwenye kundi la wanafunzi ambao hawakukidhi vigezo vya kupewa mkopo,”alisema Badru.

Alisema sio rahisi kutoa mkopo kwa wanafunzi wote, kwani Serikal inaendeshwa kwa bajeti na mwaka huu wamechagua kusomesha wanafunzi 25,000 kulingana na bajeti iliyopo pamoja na kulingana na mahitaji ya wataalamu wanaotakiwa na kutokana na vipaumbele vyake.

Alisema anatambua kuna wanafunzi zaidi ya 10,000 ambao wamekosa mikopo na kuongeza; “lakini bajeti ya mwaka huu imeishia hapo, mwaka kesho tunaweza kuishauri Serikali iongeze fedha baada ya kuwa tumefanya tathmini uhitaji wa mikopo hiyo.”

Hata hivyo, Badru alisema kuna wanafunzi ambao wanasoma kozi za kipaumbele, lakini wazazi wao wana uwezo, hao nao hawakupatiwa mikopo licha ya kuwa kwenye kundi la wanaostahili mkopo.

“Kuna mtu anasomea udaktari, lakini wazazi wake wana uwezo, na kuna mwanafunzi anasomea sayansi ya jamii na wazazi wake ni watu wasio na uwezo, hapo lazima tuangalie mhitaji ni yupi kati ya hao wawili na ndiye tunampatia mkopo,” alisema Badru.

Alisema kuna wanafunzi wanasoma kozi za kipaumbele baadhi yao hawakupata mkopo kabisa na baadhi yao wamepatiwa mkopo kidogo baada ya bodi hiyo kufanya tathmini ya hali ya uchumi ya wazazi au walezi wa mwombaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post