MWILI WA SPIKA MSTAAFU WA BUNGE LA TANZANIA SAMUEL SITTA KUWASILI KESHO ALHAMISMWILI wa Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta ambaye alifariki dunia juzi nchini Ujerumani, utawasili nchini kesho alasiri.

Mwili wa Sitta ambao utazikwa siku ya Jumamosi huko Urambo, utaagwa na wananchi wa jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akiishi, Dodoma ambako aliishi akiwa Spika wa Bunge na mjini Urambo ambako ndiko nyumbani alikokulia na kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa nyakati tofauti.

Aidha, imefahamika kwamba mwili wa Sitta utazikwa katika kitongoji cha Mwenge wilayani Urambo, eneo ambalo mwanasiasa huyo aliandaa kwa ajili ya ndugu kuzikwa.

Awali, kulikuwa na taarifa kwamba angezikwa eneo la Utemini la Wanyanyembe huko Itetemia katika Manispaa ya Tabora, kwa kuwa wamezikwa ndugu zake wengine na ndiko anakotokea mama yake, Hajjat Zuwena Said Fundikira wa ukoo wa Chifu Fundikira.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na msemaji wa familia, Gerard Mongola, mwili wa Sitta utawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 8.30 mchana.

“Baada ya kuwasili, mwili utapelekwa nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam na utalala huko hadi kesho yake siku ya Ijumaa ambako utapelekwa katika uzikwe eneo ambalo Sitta aliandaa kwa ajili ya ndugu kuzikwa".

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Peter John Sitta, awali wakati Sitta analiomba kutoka Kanisa la Moravia Urambo lilikuwa likifahamika kama Urambo Mashariki kabla ya kubadilishwa na kuitwa kitongoji cha Mwenge karibu na Uwanja wa Ndege wilayani Urambo.

Alisema eneo hilo ni nusu ekari au mita 50 kwa 50 na wakati mchakato wa kuomba eneo hilo kutoka Moravian pia walipitia na kuwasilisha maombi hayo kwa uongozi wa kijiji hicho. Alisema Sitta alifanya hivyo kwa kuona umuhimu wa ndugu waliotangulia mbele za haki, wahifadhiwe eneo hilo ili iwe rahisi kutambua nani amezikwa wapi kwa majina.

Alieleza eneo hilo tayari kuna miili iliyohifadhiwa ambako kuna kaburi la John Peter Sitta ambaye ni mwanawe na Raphael Paulo Sitta ambaye ni mtoto wa mdogo wake.

Shein amlilia

Naye Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Spika Ndugai kutokana na kifo cha Sitta, akisema amepokea kwa mshtuko na kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Sitta aliyemuelezea kuwa ni mwanasiasa aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha demokrasia na utawala bora wakati akiwa Spika wa Bunge.

Alisema yeye binafsi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar watamkumbuka Marehemu kwa ujasiri, uzalendo na mchango wake mkubwa alioutoa katika ujenzi wa Taifa na kwamba “uzalendo na umahiri wake ulidhihirika wakati alipokuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.”
 
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post