MAPROFESA WAMPINGA WAZIRI NDALICHAKO

WASOMI, wadau wa elimu na wananchi wa kawaida wamekosoa tamko la Waziri  wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakisema kwamba halijafanyiwa utafiti na halitekelezeki kisheria.

Mwishoni mwa wiki, akiwa kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Ndalichako alisema kuanzia mwakani mwanafunzi yeyote hatajiunga na masomo ya Shahada bila kupitia kidato cha sita.
Alisema mfumo wa elimu huria umechangia kuzalisha wasomi butu kwa kupokea wanafunzi dhaifu kitaaluma.
Wakizungumzia tamko hilo kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi ya wasomi  walisema kabla ya waziri kuanza kutoa amri na matamko, alitakiwa kufanya utafiti kujiridhisha juu ya agizo lake hilo.
“Profesa Ndalichako hajasema ametoa wapi ujasiri wa tamko lake, ni kwa utafiti upi aliofanya yeye au hata kukasimu taasisi kwa niaba yake ili ifanye utafiti na kuja na majibu kuwa kidato cha sita ndicho kiwango bora cha kumpitisha mtu kusoma shahada ya kwanza?
“Binafsi naona haya ni matamko ya kisiasa yasiyoweza kutekelezwa kisheria, arekebishe sheria kwanza ndio aje kutoa tamko la kurekebisha mfumo wa elimu, vinginevyo anaweza kuharibu kuliko waliomtangulia,” alisema mkuu wa chuo kikuu maarufu mkoani Arusha ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Tawi la Makumira, Mchungaji Profesa Josef Parsalao, alisema pamoja na lengo zuri la kurekebisha mfumo wa elimu, badala ya kuanza na amri na matamko, Serikali ilitakiwa kurekebisha kasoro zilizopo hatua kwa hatua.
“Sijui yeye Ndalichako alipitia hatua zipi za elimu, lakini upo ushahidi wa kuwapo kwa wasomi wengi wakiwamo wale wanaofundisha vyuo mbalimbali nchini, kupitia ngazi ya chini kabisa ya cheti na sasa ni maprofesa na walifundisha hawa wanaobeza ngazi hizo.
“Wapo majaji ambao walianza kazi ya ukarani mahakamani, wakajiendeleza kwa kusoma Chuo cha Mahakama Lushoto ngazi ya cheti, sasa ni madaktari na maprofesa wa sheria tunawategemea,” alisema Profesa Parsalao.
BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, yeye alisema haamini kama alichosema Waziri Ndalichako ni tamko na uamuzi wa Serikali, kwani suala hilo haliko kwenye sera ya elimu na kuonya kuwa alifute haraka kwani hiyo si njia sahihi ya kuboresha elimu nchini.
Dk. Bana alikwenda mbali zaidi kwa kutoa mfano wa jinsi yeye alivyosoma kupitia mfumo huo unaopingwa na Ndalichako hadi hapo alipofikia.
“Kama kachukua uamuzi huo, nafikiri amekurupuka, kama anafikiria kidato cha sita ndiyo njia pekee, ameshauriwa vibaya na huo uamuzi aufute haraka sana na ni kinyume na utaratibu wa elimu kote duniani… utakuwa ni uamuzi wa dhambi ya asili na dhambi ya ubaguzi. Kama anataka njia ya kuboresha elimu aje tumfundishe.
“Mimi binafsi sikupitia kidato cha sita na kuna maprofesa zaidi ya 20 au 40 ninaowafahamu, yupo Profesa Baregu (Mwesiga Baregu) hakusoma kidato cha sita, kuna Profesa Mathew Luhanga ambaye alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa miaka 14, yupo pia Profesa Cuthbert Kimambo ambaye alikuwa Mkuu wa Taaluma UDSM na wengine wengi, ni watu wanaoheshimika kote duniani,” alisema.
PROFESA BAREGU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, hakutofautiana na Dk. Bana. Yeye alisema mfumo uliopo unakubalika duniani kote na ndio ulioleta msemo wa ‘elimu haina mwisho’.
“Kauli ya waziri imeonyesha umuhimu wa kuwa na tume ya kitaifa ya kushughulikia suala la elimu, kwa sababu kweli kuna tatizo la ubora wa elimu yetu na halipaswi kunyamaziwa, lakini hii si njia sahihi ya kulitatua.
“Sijamwelewa waziri kwanini ameona diploma kwenda chuo kikuu ndiyo tatizo na kusema kuwa watu wote wana haki ya kujengewa mazingira ya kujiendeleza kielimu,” alisema Profesa Baregu.
PROFESA MPANGALA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema anapinga uamuzi huo wa Profesa Ndachako kwani utawanyima watu uhuru wa kujiendeleza.
Profesa Mpangala naye aliwataja baadhi ya maprofesa anaowafahamu ambao hawakupitia kidato cha sita na akasema wamekuwa msaada mkubwa kwa taifa.
“Profesa Kimambo alikuwa mwalimu wangu wa Kiswahili, yeye alikuwa na elimu ya ualimu ‘Grade’ C wa shule ya msingi lakini amejiendeleza hadi amekuwa Profesa yupo pia Profesa Ndunguru na wengine wengi na waliopitia mfumo wa Cheti-Stashahada wanakuwa na uzoefu mkubwa kuliko wa kidato cha sita na wanafanya vizuri wakifika chuo kikuu,” alisema Profesa Mpangala.
TAMONGSCO
Akizungumzia kauli hiyo ya Profesa Ndalichako, Katibu Mkuu wa Vyuo na Shule Binafsi Tanzania, Benjamini Nkonya, alisema hawaelewi waziri huyo kutoa tangazo kama hilo ni kwa sababu watu wengi wamekuwa watumishi bora sana na wengi hawajasoma kidato cha sita au vinginevyo.
“Wito wetu kwa Serikali ikamilishe mchakato kwa kupeleka rasimu ya sheria mpya ya elimu bungeni, ili pawepo na Baraza la Taifa la Elimu ambalo litakuwa na wawakilishi kutoka sekta ya umma, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na sekta binafsi kama TAMONGSCO, ambayo itaandaa nyaraka (regulations) zote kabla hazijawekewa sahihi na kamishna wa elimu,” alisema Nkonya.
PROFESA MLAMA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama, yeye alikubaliana na mawazo ya Waziri Ndalichako, akisema mfumo huo ni wa zamani na uliruhusiwa ili kutoa fursa kwa watu kusoma kwa kuwa nchi ilikuwa na wasomi wachache.
“Sasa hivi kuna wanafunzi wengi wa kidato cha sita na fursa nyingi za kusoma kidato cha tano na sita zipo, tofauti na kipindi cha miaka ya nyuma, hakuna ulazima sana wa watu kutegemea njia yingine wakati wanaweza kusoma kidato cha sita na kuwa sawa na wengine darasani,” alisema.
LALTAIKA
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ubunifu, Usimamizi wa Teknolojia na Ujasiriamali katika Taasisi ya Sayansi ya Nelson Mandela, Dk. Amani Laltaika, alipongeza hatua ya Profesa Ndalichako, huku akisema amegundua tatizo katika elimu na amethubutu kuchukua hatua ya kurekebisha kuliko waliomtangulia ambao hawakuchukua hatua yoyote.
“Sifa ya kwanza ya kiongozi ni ubunifu na kutatua matatizo yaliyopo, nampongeza waziri kwa kugundua upungufu katika elimu yetu, kwa sababu walikuwapo mawaziri wengi katika nafasi aliyopo sasa, lakini hawakugundua,” alisema Dk. Laltaika.
SIFA ZA TCU KUJIUNGA NA VYUO
Mwezi Juni mwaka huu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ilitangaza utaratibu mpya kwa watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016 na 2017 wanaochukua shahada.
Utaratibu huo mpya ulikuja baada ya miezi miwili tangu kutumbuliwa kwa watendaji wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Pamoja na sifa hizo ambazo ziliwahusu waliomaliza kidato cha sita, pia sifa hizo zilieleza kuwa wale watakaodahiliwa kujiunga na vyuo ni pamoja na watakaokuwa na utambulisho wa sifa za kielimu za kidato cha nne kuanzia alama nne ambazo ni D na kupanda juu katika mchanganuo wa alama za ufaulu wa B+, ikiwa A=75-100, B+=65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39 na F=0-38.
Sifa nyingine zinazotajwa ni wenye vyeti vya NVA daraja la tatu, wenye ufaulu si chini ya alama nne au sifa nyingine zinazokaribiana na hizo, ikiwa ni pamoja na zinazotambuliwa na Baraza ka Taifa la Mitihani (NECTA) na Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA).
Watahiniwa hao watatakiwa kuwa na angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada ‘NTA’ daraja la sita au wastani wa B kwa cheti cha ufundi ‘FTC’ katika mchanganuo wa alama A=5, B=4, C=3 na D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa wenye stashahada za ualimu au wastani wa daraja B+ kwa kitengo cha afya kama tabibu wa magonjwa ya binadamu na nyingine au cheti na stashahada nyinginezo.
Sifa nyingine zinazoangaliwa katika udahili huo ni pamoja na kuwa na ufaulu wa daraja la pili kwa wenye Stashahada zisizokuwa za NTA.
Imeandaliwa na Abraham Gwandu (Arusha), Jonas Mushi na Mauli Muyenjwa (Dar)-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post