WAKULIMA wa korosho mkoani Lindi wamefanya vituko, ikiwamo kumnunulia juisi pamoja na soda mbuzi anywe kwa kilichodaiwa haijawahi kutokea zao hilo kuuzwa kilo moja Sh 3,718 katika msimu wa mwaka huu.
Katika msimu huu wa korosho, zao hilo linauzwa kwa mnada katika mikoa ya kusini mwa Tanzania na bei yake imefikia kuuzwa zaidi ya Sh 3,700 kwa mara ya kwanza katika miaka ya karibuni, hali inayowafanya kupata kipato kikubwa kuliko miaka mingi iliyopita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rashidi Nakumbya ndiye aliyetoa siri ya wakulima kufanya vituko hivyo wakati akizungumza kwenye kikao cha viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika, wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri za wilaya na manispaa na Serikali ya Mkoa.
Nakumbya alisema kwamba hivyo ni vituko kutokana na bei kubwa ya korosho msimu huu ambayo mkulima hajawahi kuipata katika siku za karibuni, na imesababisha wakulima wengi kupata masoko mazuri, hivyo na uzalishaji utaongezeka.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Mhango alitaka wakulima wapewe elimu ya matumizi ya fedha, kwani kwa sasa wakulima wanalipwa fedha zao nyingi, lakini wanaenda kununua nyasi na kuzitoa za zamani badala ya kununua bati kujengea juu ya nyumba yake anayoishi.
Alisema si vyema wakati huo ambao wakulima wanapata fedha nyingi, kubaki katika umaskini na badala yake wajenge nyumba bora za kuishi. Alisema ni bora wabadilike hasa wakati uliopo sasa ambao kipato ni kizuri na kinapatikana.
IMEANDIKWA NA KENNEDY KISULA, -HABARI LEO LINDI