UKAWA WATINGA MAHAKAMANI KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI WA MEYA DAR


Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekimbilia mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa umeya na naibu meya wa Manispaa ya Kinondoni katika Jiji la Dar es Salaam uliompa ushindi Diwani wa Msasani, Benjamin Sitta wa CCM kuwa Meya.


Ukawa kupitia kwa Wakili wao, John Mallya wamewasilisha kesi hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 23 mwaka huu, kwa kuwa ulikuwa batili na ulikiuka taratibu za kisheria.


Mallya alisema kesi hiyo ambayo walalamikaji ni aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Jumanne Mbunju na aliyekuwa mgombea wa umeya, Diwani wa Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro, imepokelewa lakini haijafunguliwa.

Mbali na Sitta, walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya, Manyama Mangaru, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa Halmashauri hiyo.


Akizungumza baada ya kesi hiyo kupokelewa, Wakili Mallya alisema wamefungua kesi hiyo kupinga kile wanachoita uchaguzi ambao CCM walikaa wenyewe na kupigiana kura.


Alisema: “Katika kesi hiyo tunaiomba Mahakama itengue uamuzi uliomchagua meya huyo, iamuru manispaa iitishe uchaguzi wa umeya mara moja pia imuamuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa na wasimamizi wa uchaguzi wafuate taratibu za kisheria.”


Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo alisema wamefika mahakamani kutafuta haki kwa sababu wanaamini wamenyang’anywa haki yao.


Alisema kilichosababisha uchaguzi wa Ubungo kuahirishwa ni kukiukwa kwa taratibu hivyo Mkurugenzi na Ofisa Tawala wa Ubungo walipoona taratibu zimekiukwa Kinondoni, waliamua kuahirisha uchaguzi.


“Kilichofanyika siku ile ilikuwa ni kuchagua Mwenyekiti wa CCM, lakini siyo uchaguzi wa kumchagua meya wa Kinondoni kwa sababu hata kisheria, uchaguzi unatakiwa kuwa robo tatu ya wajumbe ambao walitakiwa kuwa 23, lakini walikuwa 18, ndiyo maana hata matokeo yalikuwa kura 18,” alisema.


Alidai madiwani wao walinyimwa fursa ya kuingia manispaa na kuwasilisha malalamiko yao hivyo hawamtambui Meya wa Kinondoni na kwa sasa hakuna Meya wa Manispaa hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post