SHIRIKA LA VIWANGO TANZANIA (TBS) KUFUMULIWA...VIJANA 136 KUPEWA AJIRA


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema atalifumua na kuliunda upya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kwamba wameshaanza kutafuta vijana 136 watakaoajiriwa katika shirika hilo kwa lengo la kudhibiti bidhaa, zinazoingizwa nchini chini ya viwango.


Aidha, wataweka kitengo maalumu kwa vijana hao, watakaokuwa na uwezo wa kuchunguza mipaka ya nchi, kunusanusa katika bandari bubu, kukamata, kuwasiliana na Polisi na kusimama mahakamani kutoa ushahidi.


Mwijage aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa utoaji wa tuzo kwa washiriki wa Programu ya Kaizen iliyo chini ya Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.


Alisema lengo la kuiunda upya TBS ni kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika ipasavyo ili kulinda viwanda vya ndani, vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.


“Tutahakikisha kwamba hakuna bidhaa zitakazoingia bandarini bila ya kuwa na viwango vinavyotakiwa. Lengo ni kuwalinda walaji na viwanda vyetu, kwa nini tuagize vitu nje wakati viwanda vyetu vinazalisha bidhaa,’’ alisema Mwijage.


Hatua yake hiyo imekuja siku chache, baada ya makontena 100 kutoroshwa katika bandari kavu za Dar es Salaam bila ya kukaguliwa na hivyo kuikosesha mapato serikali na pia kuwa na hatari ya kuingiza bidhaa zilizo chini ya kiwango.


Akizungumza utekelezaji wa agizo la Mwijage na hadi Jumanne wiki hii kwa waliotorosha makontena hayo kujisalimisha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Egid Mubofu alisema jana kuwa waziri ameongeza siku za utekelezaji wa agizo lake la kuwataka wafanyabiashara walioingiza maontena 100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, watoe taarifa.


Dk Mubofu alisema baada ya agizo la awali, lililokuwa linamalizika Jumanne Oktoba 18, waziri aliongeza hadi leo ndipo hatua stahiki zichukuliwe.


Hata hivyo, alisema mwitikio umekuwa mkubwa na baada ya majumuisho ya leo, atakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa taarifa kuhusu suala hilo.


Septemba 13, Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, wakatoe taarifa katika shirika hilo.


Mwijage alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.


Akizungumzia Programu ya Kaizen, Waziri Mwijage alisema jambo linalotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba viwanda vingi, vinakuwa na mfumo huo wa Kaizen, kwani utasaidia kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango vya hali ya juu.


Alisisitiza lazima wafanyabiashara waboreshe bidhaa zao na kwamba wasitengeneze bidhaa kumtosheleza mteja bali kumridhisha mteja.


“Hatutaki kuingiziwa bidhaa ‘midabwada’ wala mataputapu, tunachotaka ni bidhaa zenye viwango vinavyotakiwa na tunataka wazalishaji wetu mzalishe bidhaa zenye viwango na viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi,’’ alifafanua.


Hata hivyo, alisema sababu ya viwanda kufa ni baada ya kufunguliwa milango ya bidhaa kutoka nje kuingia nchini, ambazo hazikukidhi viwango na kwamba wafanyabiashara kutoka nje walikuwa wanashindana na wafanyabiashara waliopo, ambao waliwekeza fedha nyingi katika miradi yao.


Kwa mujibu wa Mwijage, mpango huo wa Kaizen umefanywa katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma ambapo umesaidia kuongeza tija katika uzalishaji na kupunguza upotevu wa malighafi.


Aidha, aliwataka Watanzania kupenda vitu vya nyumbani kwani wanahakikishiwa ubora na endapo vitakuwa na tatizo ni rahisi kuwabana wafanyabiashara wa ndani kuliko wa nje.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa JICA nchini, Toshio Nagase alisema mpango huo umesaidia kufundisha wakufunzi kwenye kampuni na viwanda zaidi ya 50 vilivyopo nchini.


Nagase alisema Kaizen imeleta matokeo kwa vitendo kwenye maeneo ya biashara kwa njia ya kusafisha eneo, kupunguza malighafi, kuhakikisha ubora wa bidhaa na kubadilisha tabia au motisha kwa wafanyakazi.


‘’Tunaamini kwamba Kaizen ni jambo muhimu katika kutengeneza viwanda vyenye ushindani kibiashara na kufanikisha lengo la kukuza viwanda kuelekea mwaka 2025,’’ alisema.


Alisisitiza kuwa mradi huo wa miaka mitatu, ulianza mwaka 2013 na kwamba ulianza Japan na nchi za Afrika unatekelezwa katika nchi za Ethiopia, Tunisia, Misri, Ghana, Zambia na Tanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post