MTUHUMIWA "PANYA ROAD" AZINDUKA MOCHWARI BAADA YA KUPIGWA NA WANANCHI MTOTO aliyetambuliwa kwa jina la Isack Ernest (16) anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi cha uhalifu cha ‘panya road’ amezinduka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.


Ernest, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na mkazi wa Buza, anayedaiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi hicho, alidhaniwa amekufa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuwaibia mali zao.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna vijana watatu wamekufa katika eneo la Mbagala na baada ya kufika eneo la tukio waliwakuta vijana hao wakiwa na hali mbaya.

Kamanda Muroto alimtaja mmoja aliyejulikana kwa jina la Kelvin Nyambocha (14) kuwa alikufa baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi na kwamba kabla ya mauti kumkuta alifuatana na wenzake kwa ajili ya kwenda kuangalia tamasha la muziki wa Singeli lililofanyika Mbagala Zakhem.

Kijana mwingine Selemani Hamis (16), mkazi wa Kilingule, alifariki akiwa chumba cha upasuaji katika hospitali ya wilaya Temeke.

“Wakati watu wanarudi kutoka katika tamasha hilo, kundi la vijana hao walianza kuwavamia watembea kwa miguu na kuanza kuwaibia mali zao na ndipo wananchi waliwakamata hao watatu na kuanza kuwapiga,” alisema Kamanda Muroto.

Alifafanua kuwa Ernest alipigwa hadi kuzimia na wananchi hao walijua kuwa amekufa ambapo alipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo kuwekewa namba na kuingizwa kwenye jokofu.

“Wakati mwili wake umewekwa chini kabla ya kuingizwa kwenye jokofu, alipumua na kuzinduka na kuonekana kuwa bado yupo hai hali iliyosababisha kupelekwa chumba cha uangalizi maalumu wa madaktari,” alisema.

Kamishna Muroto alisema baada ya kupata fahamu na afya yake kutengemaa alihojiwa na kuwataja wenzake 10 ambao yuko nao katika kundi moja.

Alisema kijana mwingine fundi magari aitwaye Faraji Suleiman (19) mkazi wa Buza Kwa Rulenge, hali yake ni mbaya na amelazwa katika Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Alisema Polisi kupitia Sheria ya Watoto ya Mwaka 2009 kifungu 7/9, wazazi wana wajibu wa kuhakikisha mtoto anakuwa chini ya uangalizi wao, hawawekwi kwenye mazingira yatakayowasababishia madhara ya kimwili pamoja na kisaikolojia.

Alisema kuwa jukumu la mzazi ni kuhakikisha mtoto anakua kwenye malezi bora na sio kumuacha kwa walimwengu.

Aidha, alitoa mwito kwa mzazi yeyote kumsimamia vyema mtoto wake na kukiuka Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 kifungu cha 14 na kwamba atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atafungwa miezi 6 au kulipa faini ya Sh milioni tano.

Alisema kwa mazingira waliyokutwa watoto hao, wazazi wao ni watuhumiwa kwa kukiuka sheria hiyo ya watoto.

Awali taarifa ya Polisi, Temeke ilieleza kuwa inawashikilia vijana 16 wanaodaiwa ni wa kundi la uhalifu la ‘panya road’ liitwalo ‘taifa jipya’ kwa kuhusika kuwavamia watu kwenye tamasha la kuinua vipaji, la Oktoba 15 mwaka huu.
Imeandikwa na Yusuf Badi na Katuma Masamba -Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post