MTUHUMIWA AJINYONGA KWA ZIPU KATIKA KITUO CHA POLISI

 
Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Andrew Satta

MTUHUMIWA wa kosa la kunajisi, Mwita Makwabe (52) amekutwa amejinyonga chooni akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Sirari.


Mtuhuhimiwa huyo amejinyonga kwa kutumia zipu ya koti lake. Alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kumnajisi mtoto wa kike wa miaka sita.

Makwabe alikuwa mkazi wa kijiji cha Ng'ereng'ere, kata ya Regicheri, tarafa ya Inchugu, wilayani Tarime, Mara.

Kamanda wa Polisi wa Tarime/Rorya, Andrew Satta, amethibitisha tukio hilo.

“Makwabe alikamatwa mwishoni mwa wiki katika mpaka wa Sirari na Isebania akimnajisi mtoto mdogo wa kike ambaye alisikika akipiga kelele za kuomba msaada. 
Wananchi wakishirikiana na askari wa Kenya walijitokeza na kumkamata mtuhumiwa huyo na kumkabidhi kwa askari. 
Alifikishwa kituoni kwa mahojiano zaidi ambapo mtoto huyo (jina limehifadhiwa) aliyekuwa ameumizwa vibaya na mtuhumiwa alipelekwa hospitali," amesema Kamanda Satta.

Amesema usiku wa kuamkia jana, mtuhumiwa alichana koti lake na kutoa zipu na kuingia chooni na kufunga zipu hiyo kwenye nondo za dirisha la choo na kujinyonga.

Aligundulika na mahabusu wenzake alfajiri akiwa ameshakufa.

Kamanda Satta amesema mtuhumiwa alikuwa afikishwe mahakamani jana kujibu mashitaka ya kumnajisi mtoto huyo.

Mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya kwa uchunguzi.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post