MTENDAJI WA KATA MBARONI KWA KULAMBA PESA ZA WANANCHI



MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Juma Mhina ameamuru polisi wa wilaya hiyo kumkamata na kumweka ndani mtendaji wa kata ya Gelai Lumbwa, Paulo Lucas, kwa kutuhumiwa kutumia vibaya fedha zilizochangwa na wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kuinua sekta ya elimu.

Baada ya Lucas kuwachenga polisi mara kwa mara, hatimaye jana agizo hilo lilitekelezwa katika maeneo ya kijiji cha Ilchang Sapukin, kata ya Gelai Lumbwa, kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Kabla ya Lucas kukamatwa, mwananchi Anni Mollel alimshukuru Gambo kufika katika eneo lao kujionea hali halisi ya ujenzi wa shule ya sekondari ambayo wananchi walichanga fedha zao zaidi ya Sh milioni 96 lakini hazikutumika kama ilivyokusudiwa, badala yake viongozi wa serikali na wenyeviti wa vijiji walizitumia kujinufaisha.

Baada ya Mollel kuzungumza, Gambo alimuuliza Mkurugenzi Mhina ni kwa nini hawajachukua hatua za kisheria kuwakamata watuhumiwa, ndipo Mhina aliposema mbele ya hadhara hiyo kuwa agizo lilishindikana awali baada ya Lucas kumkwepa mkurugenzi huyo mara kwa mara.

Alikamatwa jana katika mkutano huo. Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo, Mwajuma Mndaira katika taarifa yake aliyoitoa mkutanoni hapo alisema alifanya mahojiano na wenyeviti wa vijiji kujua ni kwa nini walikusanya fedha kwa wananchi pasipo kutumia risiti za stakabadhi.

Alisema pia hivi sasa bado wanaendelea na uchunguzi wa nyaraka na malalamiko ili kubaini Lucas alihusika pamoja na akina nani na kwa nini abadilishe baadhi ya matumizi kwani baadhi ya kampuni za uwindaji wa kitalii ikiwemo Wingert Windrose Safaris (WWS) na kampuni ya Kilombero Northern Safaris zilitoa mifuko ya saruji 400 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari.

Alisema wakati walipokuwa katika eneo hilo panapojengwa shule ya sekondari walibaini kuwa licha ya mifuko hiyo ya saruji kutolewa, 44 tu ndio iliyotumika huku mifuko 144 ikiwa imeuzwa na mifuko mengine 216 walidai walitumia kwenye ujenzi wa maabara na madarasa yaliyokuwa chakavu.

Pia baada ya kufanya ukaguzi huo awali alimwelekeza Mhandisi Ujenzi kufika kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuthaminisha ujenzi huo ili kubaini ni kweli ilitumika katika ujenzi huo au la, kwani mtendaji huyo alitoa baadhi ya malighafi na kuziuza huku akijua kuwa ni kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Gambo alimhoji mtendaji huyo kuwa ni kwanini wananchi hawana shule ya sekondari.

Alisema watoto wa jamii ya kifugaji na wengine wanahitaji elimu na wanatembea umbali mrefu kutafuta elimu wakati yeye (Lucas) na viongozi wengine wakitumia hela za wananchi vibaya.

Lucas akijitetea, alisema kuwa fedha hizo zilitumika kihalali na baadhi ya fedha alilazimika kubadilisha matumizi yake na kujenga vyumba vya maabara, jiko, mabweni na kadhalika.

Aliendelea kujitetea kuwa fedha hizo alizitumia yeye na viongozi wengine kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule ya sekondari ambayo bado haijakamilika.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post