MAKONDA AWAGEUKA MACHINGA DAR,AWAPA SIKU 14 KUONDOKA BARABARANI
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku 14 kwa wakuu wa wilaya kuhakikisha wanawapatia sehemu ya kufanyia biashara wamachinga wote wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara.

Pia amewataka wale ambao tayari wamepatiwa maeneo kurejea katika maeneo yao na kuondoa biashara zao pembezoni mwa barabara.

Makonda alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa ambapo aliwataka wafanyabiashara hao kutoitumia vibaya kauli ya Rais John Magufuli kwa kuwa tayari wameshatengewa maeneo lakini waliamua kurejea baada ya kauli hiyo.

“Rais wetu alisema wasibughudhiwe ila watengewe maeneo maalumu kwa ajili ya kufanyia biashara zao, maeneo tumeshatenga hivyo ni vyema wakarejea katika maeneo yao na wale ambao hawana kabisa waonane na wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ili wapatiwe maeneo,” alisema.

Alisema uwepo wa wafanyabiashara hao katika maeneo ya hifadhi ya barabara kumesababisha kero na misongamano isiyo ya lazima inayowanyima uhuru watembea kwa miguu.

“Hatukuweka lami ili utandike bidhaa zako barabarani, watembea kwa miguu wanateseka kwa sababu yenu vibaka wameongezeka watu wanaibiwa kila kukicha nitoe wito tu muondoke wenyewe na hatutapenda kutumia nguvu kuwaondoa,” alisema Makonda.

Aliongeza kuwa kuwepo kwa wamachinga hao kumeisababishia Manispaa ya Ilala kupoteza mapato kwa kuwa kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waaminifu wakiwatumia wafanyabiashara hao kuuza bidhaa zao na kukwepa kulipa kodi.

“Wamachinga wamekuwa wakitumika kupitisha mizigo kwa njia zisizo sahihi, kuna watu wanawakusanya na kuwapeleka kwa wafanyabiashara wakubwa na kuwapatia bidhaa jambo linalosababisha bidhaa hizo kuuzwa bila kulipiwa kodi,” aliongeza Makonda.

Aidha Makonda alisema jiji hilo lina mpango wa kuweka maeneo maalumu yanayoonesha bidhaa za ndani na zile zinazotoka nje ya nchi.

Imeandikwa na Sophia Mwambe-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post