MADAKTARI WATUMBULIWA KWA UZEMBE,MAZOEA NA KUTOWAJIBIKA KWA WANANCHI


NB-Siyo picha ya madaktari waliotumbuliwa
***
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro, Marcelin Ndimbwa amewasimamisha kazi Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Matimbira, Dk Severiana Mayenja, Daktari wa zamu, Dk Evelyne Tenes na Tabibu wa zamu, Nsallu Masembo kwa tuhuma ya kufanya uzembe, mazoea na kutowajibika ipasavyo katika kutoa huduma kwa wananchi kulikokithiri.

Amechukua hatua hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho cha afya kuanzia saa 5:55 hadi 8:45 usiku juzi ambako alimkuta mjamzito, Doreen Konga akiwa katika hali mbaya huku mwili wake ukiwa umeanza kubadilika rangi kwa ajili ya maumivu baada ya kushindwa kujifungua.

Mkurugenzi huyo anadai kuwa mgonjwa huyo alitelekezwa na mganga wa zamu.

Katika ziara hiyo, mkurugenzi huyo alifuatana na Ofisa Utumishi wa Wilaya, Bhango Lyangwa, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Idd Mujungu na alitaka kujiridhisha na hali ya uwajibikaji ya watumishi kwenye kituo hicho kwani amekuwa akipokea malalamiko ya muda mrefu na mfupi kutoka kwa raia wema na kuangalia namna ya kuyatatua kwa haraka zaidi.

Hii ni mara ya pili kwa mkurugenzi huyo kutembelea kituo hicho kwani alifanya ziara ya kushitukiza Agosti 10, mwaka huu saa 6:00 usiku na hakukuta tabibu yeyote wala muuguzi huku wagonjwa sita wakiwa wameishiwa dripu za dawa kwa zaidi ya saa mbili.

Mkurugenzi huyo alipofika katika kituo hicho akiwa na ofisa utumishi wa wilaya na mganga mkuu wa wilaya, walimkuta muuguzi wa zamu, Martha Hiiti na baada ya mahojiano alimweleza mkurugenzi huyo na ujumbe wake kuwa saa 3:00 usiku alimwita daktari wa zamu kumwarifu habari za mgonjwa huyo, lakini hakuonekana hadi ilipofika 5:15 usiku; na alipofika alitoa fomu ya rufaa na kumwamuru aijaze fomu ya rufaa bila kumhudumia mgonjwa na kuondoka.

Mganga wa zamu, Nsallu Masembo hakuwepo kituoni hapo na alipopigiwa simu, hakupokea hadi alipofuatwa na mlinzi usiku huo nyumbani kwake.

Muuguzi huyo aliwaeleza viongozi hao kwamba aliachwa aendelee na huduma bila kusaidiwa na daktari wala tabibu wa zamu na akishindwa aandike rufaa.

Baada ya jitihada za kuwatafuta madaktari kushindikana na kwa viongozi na muuguzi kupokezana kwa simu, mkurugenzi aliamuru mgonjwa aliyekuwa na hali mbaya, kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Malinyi ya Lugala. Baada hapo, aliamua kuwasimamisha kazi wafanyakazi hao wa kituo cha afya na akaunda tume ndogo ya uchunguzi.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post