BAADA YA KUFUTIWA MASHTAKA...SCORPION AFUNGULIWA MASHTAKA UPYA


SALUM Njwete ‘Scorpion’ ambaye anadaiwa kumtoboa macho Said Ally, leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar kwa mara ya tatu na kufutiwa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili awali na kufunguliwa mashitaka mapya.
 
Awali Scorpion alikuwa akikabiliwa na shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo leo majira ya saa tatu na nusu asubuhi alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Adolf Sachole ambaye alisema upande wa mashitaka umeridhia kuliondoa shauri hilo mahakamani hapo kwa kutumia kifungu kidogo cha sheria namba 91 na kufutwa kesi hiyo.
 
Baada ya hakimu Adolf kusoma shitaka hilo mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote na alirudishwa rumande mpaka ilipofika saa sita na robo mchana ndipo alipotolewa tena na kupandishwa tena kizimbani baada ya kufunguliwa shitaka jipya la unyang’anyi kwa kutumia silaha.
 
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Chensesia Gavyole alisema mbele ya hakimu Flora Haule kuwa mnamo Septemba 6 mwaka huu maeneo ya Buguruni, Scorpion alimpora Said fedha, cheni ya dhahabu na kumjeruhi kwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo tumboni na begani.
 
Katika shitaka hilo jipya Scorpion baada ya kutakiwa kujibu kama kweli alitenda kosa hilo au si kweli alisema si kweli pia alilikana jina la Scorpion na kusema kwa msisistizo kuwa jina lake ni Salum Njwete Salum.
 
Baada ya hapo Scorpion alirudishwa rumande na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena mahakamani hapo Novemba 2 mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post