MGEJA AWATAKA VIGOGO WA SERIKALI KUJIUZULU KWA KUSHINDWA KUMSHAURI RAIS MAGUFULI..YUMO JAJI MTUNGI NA MWAKYEMBE






MWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja amemtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, wajiuzulu kwa kile alichodai kuwa wameshindwa kumshauri Rais John Magufuli katika masuala yanayohusu Katiba na Sheria.

Mgeja pia amepinga kauli ya Rais Magufuli kutaka kupiga mnada majengo ya serikali baada ya kuhamia Dodoma.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mgeja alisema watu hao wameshindwa kuzitumikia vema nyadhifa zao kumshauri Rais katika masuala ya Katiba na Sheria na kusababisha mvutano mkubwa unaochagizwa na kuvunjwa kwa haki za katiba za vyama vya siasa kufanya shughuli zao.

Alisema ingawa watu hao ni wasomi waliobobea katika masuala ya Sheria na Katiba lakini wameshindwa kutekeleza wajibu wao.

“Kama wamemshauri Rais kuhusu masuala ya Katiba na Sheria ambayo yamesababisha mvutano katika jamii naye hakuwakubalia basi niwaombe wawe waungwana wajiuzulu kulinda heshima zao,” alisema Mgeja.

Mgeja aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuhamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alisema jambo hilo si geni kwa kuwa hata wakati wa awamu ya kwanza, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Edwin Mtei alijiuzulu baada ya kukataliwa ushauri wake na rais wa wakati huo, Mwalimu Nyerere kuhusu masuala ya IMF.

“Viongozi hawa walikuwapo tangu serikali zilizopita na wanajua sababu ya kuacha kuzuia shughuli za siasa lakini wameshindwa kutumia uzoefu wao kumsaidia Rais, lolote litakalotokea baya watakuwa wameshiriki,” alisema Mgeja.

Alisema kukaa kimya kwa viongozi hao katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliwa na kukiukwa katiba na sheria mbalimbali, hawawatendei haki wananchi licha ya dhamana waliyopewa na Rais.

NA TUNU NASSOR- DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527