Picha na Audio: Kamanda Mpya Wa Polisi Shinyanga Aanza Kazi Kwa Kasi ya Ajabu..Askari Wanaobambikizia Kesi Raia Kukiona Cha Moto


Julai 21,2016 saa nne asubuhi Kamanda mpya wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro (pichani) amekutana na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga katika ofisi yake mjini Shinyanga kwa ajili ya kujitambulisha na kuwaeleza mikakati mbalimbali aliyoipanga kuhakikisha kuwa vitendo vya kihalifu vinakwisha mkoani Shinyanga. Mwandishi Mkuu wa Mtandao huu ,Kadama Malunde,anaripoti.

Miongoni mwa mambo aliyoyasisitiza ni pamoja askari polisi kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia weledi, kanuni na sheria.

Kamanda huyo ametumia fursa hiyo kuwaonya askari ambao wamekuwa wakiwabambikizia kesi wananchi ambao siyo walengwa wa matukio husika kwa tamaa ya rushwa waache tabia hiyo mara moja na atakayebainika atachukulia hatua za kinidhamu.

Amewasisitiza askari polisi kuhakikisha wanaepuka vitendo vya kubambikizia kesi raia hali inayosababisha askari polisi wote Shinyanga waonekane hawafai na raia kutokuwa na imani na jeshi la polisi.

Kamanda huyo amewataka askari polisi watende haki kwa kila raia na kuhakikisha kuwa wanazuia uhalifu kabla ya kutendeka badala ya kukimbizana baada ya matukio kujitokeza.

Murilo amewataka askari polisi kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii kutokana na vitendo vyao,lugha zao,majukumu yao na kuhakikisha kuwa wanajiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikilitia doa jeshi la polisi.

Kamanda Jumanne amesema ili kuhakikisha mikakati aliyojiwekea inafanikiwa kila mwezi kutakuwa na baraza la askari kwa kuchambua kupata ofisa wa polisi aliyefanya kazi vizuri na kumpatia zawadi na anayefanya vibaya kuliko wote kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Kamanda huyo amebainisha kuwa tayari amekutana na viongozi mbalimbali wa jeshi hilo kwa ajili ya kukumbushana majukumu ya kikazi.

Amesema atahakikisha anafanya kazi kwa weledi kwa kushirikiana na askari wote,wananchi,waandishi wa habari na wadau wote wa maendeleo na kuwa atahimiza kufanyika kwa upelelezi wa makosa mbalimbali kwa haraka ili kubainika ukweli na mtu anayetuhumiwa na kosa achukuliwe hatua asiyehusika asibambikiziwe kesi.


Amesema ataendeleza mapambano dhidi ya mauaji ya vikongwe vinavyosababishwa na waganga wa kienyeji kuendesha vitendo vya ramli chonganishi huku akiwahamasisha waandishi wa habari kushirikiana na jeshi la polisi kuielimisha jamii kuondokana na dhana potofu zinazosababisha vifo vya watu wasio na hatia.


Kuhusu tabia ya baadhi ya makamanda kuwa na tabia ya kuficha baadhi ya taarifa za kihalifu kwa waandishi wa habari, kamanda Jumanne amesisitiza kuwa yeye ni muwazi hivyo hataficha taarifa yoyote kwa waandishi wa habari.

Malunde1 blog inakusogezea sauti ya Kamanda Muliro Jumanne wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Julai 21,2016...Amezungumza mambo mazito hakika kama ataungwa mkono na wadau wote wa amani,vitendo vya kihalifu vitapungua kwa kiasi kikubwa ama kumalizika kabisa mkoani Shinyanga..Sauti iko chini ya picha hizi hapo chini.


Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akisalimiana na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club) bwana Kadama Malunde (kushoto)
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akijitambulisha kwa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ofisini kwake leo,siku chache tu baada ya kuteuliwa na mheshimiwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuongoza jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga.
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga leo
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga...Aliyevaa nguo ya bluu ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga bwana Kadama Malunde,ambaye pia ni mkurugenzi wa Malunde1 blog
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga
Waandishi wa habari wakiandika dondoo muhimu
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari
Waandishi wa habari wakimsikiliza kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro
Waandishi wa habari wakiwa kwenye ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga

Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga. Kulia ni Mratibu wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga bi Nunu Abdul


Nimekurekodia sauti ya Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro  wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo Julai 21,2016..Sikiliza Hapa chini


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post