Dereva wa Basi la City Boy Asomewa Mashitaka 30 ya Kuua Watu 30


MMOJA wa madereva waliosababisha ajali ya mabasi ya City Boy Jumatatu iliyopita katika kijiji cha Maweni wilayani Manyoni, Jeremiah Semfungwe (34), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na makosa 30 ya kuua bila kukusudia.


Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joyce Minde, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Semfungwe alitenda makosa hayo Julai 4 mwaka huu saa 8.15 mchana wakati akiendesha basi T. 247 BCD mali ya Kampuni ya City Boy kwa kuligonganisha na basi T.331DCE.


Wakili Mkuu Mfawidhi wa Serikali, Zakaria Ndaskoi alidai kuwa siku ya tukio mshitakiwa ambaye ni dereva na mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, bila kukusudia, alisababisha vifo vya abiria 30 kinyume na Kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Toleo la Kwanza.


Wakili wa mshitakiwa, Francis Kitope aliiomba mahakama impe mteja wake dhamana kwa kuwa chini ya Kifungu 148 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kosa hilo linadhaminika.


Hata hivyo, Wakili wa Serikali Ndaskoi alipinga hoja hiyo kwa kudai kuwa kwa kufanya hivyo usalama wa mshitakiwa utakuwa hatarini kwa kuwa ndugu wa marehemu na majeruhi bado wana hasira kutokana na ajali hiyo kuwa bado “mbichi”.


Aidha, Ndaskoi ambaye alikuwa akisaidiana na Petrida Muta aliendelea kudai kuwa majeruhi 54 wa ajali hiyo hali zao bado ni mbaya na hatma yao haijulikani hivyo si vyema mshitakiwa kupewa dhamana na kwamba mshitakiwa mwingine, dereva Boniface Mwakalukwa ametoroka.


Mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka juu ya kesi za mauji na ameswekwa rumande hadi Julai 21 kesi yake itakapotajwa tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post