Serikali : “Mapenzi ya Jinsia Moja..Hayakubariki .. ni Kinyume na Sheria ya Tanzania”

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Amon Mpanju amesema kuwa mapenzi ya jinsia moja hayakubaliki na Serikali ilishaweka msimamo wake katika hilo.




Akizungumza mapema leo katika mkutano wa wadau wa haki za binadamu uliofanyika katika hoteli ya Blue Pearl wa kujadili mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu (Universal Periodic Review), Mhe. Mpanju ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo alisema mapendekezo yaliyowasilishwa Mwezi Mei mwaka huu katika mkutano wa Baraza la haki za binadamu uliofanyika Geneva, serikali ilikubali mapendekezo Mia thelathini (130) na mengine 72 iliyakataa.



“Sehemu ya mapendekezo hayo serikali iliyakataa kwa sababu kuna mengine yapo kinyume na katiba, sheria, mila na desturi zetu, kwani katika mapendekezo hayo yapo yanayotaka mapenzi ya jinsia moja jambo ambalo haliwezi kukubalika”, Mhe. Mpanju alisema



“Hivyo wakati mkijadili namna ya kupanga mikakati ya utekelezaji ili serikali ione umuhimu wa kukubali sehemu ya mapendekezo hayo naomba msijielekeze kwenye yale yaliyo kinyume na imani”, Mhe. Mpanju alisisitiza



Aidha, Mhe. Naibu Katibu huyo alisema serikali imefungua milango kwa kushirikiano na tume, wadau wa haki za binadamu wapeleke serikalini sababu zenye mantiki ili kuona ni mambo gani ambayo serikali inaweza kuyashugulikia na kuyatekeleza.



Akizungumza katika Mkutano huo, Bwana Onesmo Olengurumwa kutoka taasisi ya watetezi wa haki za binadamu (THRDC) alisema kuwa wadau wamekutana katika mkutano huo kujadili ni kwa namna gani wataishawishi serikali ili iweze kuyakubali mapendekezo yaliyobakia na kuyaweka katika utekelezaji.



Akifungua mkutano huo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Iddi Mapuri alisema kuwa mkutano huo umelenga katika kuweka mikakati ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo hayo na alipongeza mchango mkubwa unaotolewa na wadau wa haki za binadamu katika kuhakikisha masuala ya haki za binadamu yanapata msukumo mkubwa hapa nchini.

Bwana Onesmo Olengurumwa (aliyevaa koti la Drafti) kutoka taasisi ya watetezi wa haki za binadamu (THRDC) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Idara ya huduma za sheria wa Tume ya Haki za Binadamu, Bwana Nabor Assey( aliyevaa shati la bluu). Nyuma yao ni Bwana Laurent Burilo burilo, Mratibu wa Mpango kazi wa Haki za Binadamu(katikati) na Bwana Deugratius Bwire kutoka (THRDC


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Amon Mpanju (aliyevaa miwani) akiteta jambo na Bwana Onesmo Olengurumwa (aliyevaa koti la Drafti) kutoka taasisi ya watetezi wa haki za binadamu (THRDC) katika mkutano huo wa kujadili mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu na kuweka mikakati ya kuishawishi serikali kukubali mapendekezo mengine ambayo iliyakataa.


Sehemu ya wadau wa haki za binadamu wakifuatilia majadiliano katika mkutano huo wa kujadili mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527