CCM Yawalima Barua Wabunge Wake Wasiohudhuria Bungeni,Wanaochelewa na Wanaoondoka Mapema


Kamati Kuu ya CCM imeagiza Kamati ya Wabunge wa chama hicho kuwapa barua za kujieleza wabunge wao wasiohudhuria, wanaochelewa na wanaondoka kabla ya vikao vya Bunge kuahirishwa.


Tayari maagizo hayo yamefanyiwa kazi na Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza ambaye amewalima barua wabunge hao.

Katika barua yenye kichwa cha habari “Maagizo ya Kamati Kuu ya CCM” aliyopewa mmoja wa wabunge wa CCM inaonyesha wametakiwa kujieleza kwa nini siku nyingine walifika wamechelewa na mara kadhaa walitoka mapema kabla kuahirishwa kwa Bunge.


“Mwenendo huu ni kukiuka kanuni za Kamati ya Wabunge wote wa CCM hasa kanuni ya 41. Tafadhali andika maelezo kwa nini Kamati Kuu isichukue hatua? Maelezo yanifikie kabla ya Juni 25 mwaka huu,” ilisema sehemu ya barua ya mmoja wa wabunge walioandikiwa.


Alipoulizwa Rweikiza kuhusiana na barua hiyo alisema haitambui na kwamba imeghushiwa.

“Kanuni zipo zinazoongoza vikao vya Bunge, zipo pia zinazoongoza wabunge wa CCM.


"Wakitaka kuondoa wabunge wa CCM wanazijua sana, isipokuwa hatujafikia hatua ya kufundishana kwa kuanza kuandikiana barua,”alisema.


“Wanajua mbunge hawezi kuondoka bila kwenda kwa Spika na kuomba ruhusa au kujulisha kwenye chama kwamba anatoka, wanajua,” alisema Rweikiza na kusisitiza kwamba hata taarifa zinazoonyesha kuna wabunge wanaotakiwa kujieleza kwake ni majungu tu.


Japokuwa Rweikiza ameikana barua hiyo, wabunge kadhaa wa CCM walioomba majina yao yasitajwe wamekiri kwamba barua hizo zimetolewa na kwamba wanabanwa kwa kutakiwa kujisajili mara mbili; kitabu cha Bunge na cha CCM.


Katika ukurasa wake wa Facebook uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema wabunge wa CCM wanalalamikia kulazimishwa kuingia bungeni kwa kuwa Bunge halina ladha.


Pia, Msigwa alisema wabunge hao wa CCM wanadai Naibu Spika Dk Tulia Ackson hafuati kanuni na taratibu na kwamba wametakiwa kujieleza Kamati Kuu ya CCM.


Aidha, baadhi ya wabunge wa CCM walionekana kukerwa na utaratibu wa kujisajili sehemu mbili yaani Bunge na CCM mara mbili kwa siku.


“Kuna haja gani ya kutia dole (kusaini kwa utaratibu wa kieletroniki) halafu tena tuje tusaini kwenye makaratasi ya CCM?,” alihoji mmoja wa wabunge.


Alisema ili kusaini karatasi hizo inawapasa wabunge kwenda upande wa Kambi Rasmi ya Upinzani ambapo wabunge waliokabidhiwa kazi ya kuzitunza karatasi hizo hukaa kama kambi mbadala baada ya wabunge wa upinzani kususia vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia.


“Wengine tunaheshima zetu hatuwezi kwenda upande wa upinzani kufuata makaratasi ya kusaini. Kwanza Bunge lenyewe halina mvuto unakuja hapa watu wawili ndio wanapewa nafasi ya kuchangia mjadala na baada ya hapo wanapitisha,” alisema.


Mbunge mwingine wa CCM alisema haoni haja ya kuwepo ndani ya Bunge kwa sababu hawapewi nafasi ya kutosha ya majadiliano na hivyo bora kutokuwepo ndani ya ukumbi muda wote.


“Mimi saa hizi naingia ndani ya ukumbi wa Bunge nasaini natoka naenda zangu kantini (ya Bunge) kuangalia mpira maana hata nikikaa ndani sitopata nafasi ya kuchangia,” alisema mbunge huyo.


Alisema haoni haja ya kusaini mara mbili kwa sababu CCM wanaweza kutumia usajili wa Bunge kufahamu wabunge waliopo na wasiohudhuria kwa wakati wanaouhitaji.

Alisema orodha hiyo haina mashiko kwa sababu wanazo namba za wabunge wote kama kuna jambo ambalo wanahitaji basi wanaweza kuwataarifu.


“Hata mimi nimepewa barua ya kujieleza lakini si kwamba ni mtoro bali tunakuwa na majukumu mengine ya kibunge nje ya Bunge,” alisema.


Hatua hiyo inakuja wakati wabunge 118 wa vyama vinavyounda Ukawa, wakiwa wamesusia vikao vya Bunge vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa madai ya kuongoza vikao kibabe na kutofuata kanuni.


Hii ni wiki ya nne tangu Dk Tulia aanze kuendesha vikao vya Bunge peke yake bila kupokewa na wenyekiti wa Bunge kama ilivyokuwa kabla hajatofautiana na kambi rasmi ya upinzani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post