Afariki Dunia Baada ya Kubugia Pombe Haramu Aina ya "Gongo" Huko Mwanza



MKAZI wa Mondo katika Kijiji cha Kitumba wilayani Magu, Wilson Magola (45), amekufa baada ya kunywa pombe haramu ya gongo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoani Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea Juni 23, mwaka huu, saa 8:00 mchana kitongojini humo.


Msangi alieleza kuwa, baada ya kufika nyumbani kwa Daudi Mtula anayeuza gongo kwa siri Magola alikunywa pombe hiyo kupita kiasi akaishiwa nguvu na kupoteza maisha.


“Mtu huyo pia alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa,” Kamanda Msangi alisema na kuongeza kuwa, baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka na kuuacha mwili wa marehemu nyumbani kwake.


Alisema kuwa Polisi inamtafuta kwa ajili ya kumchukulia hatua za kisheria.


“Tulipata taarifa kutoka kwa raia mwema na tulipofika nyumbani kwa mtuhumiwa tuliupata mwili na tayari umekwishafanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya maziko,” alisema.


Alitoa wito kwa wananchi kuiunga Polisi mkono kudhibiti biashara ya pombe hiyo haramu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527