Trump njia nyeupe uteuzi wa Republican,Hasimu Wake Mkuu Ted Cruz Ajitoa Katika Kinyang'anyiro

Njia ya Donald Trump kupeperusha bendera ya chama cha Republican katika uchaguzi wa rais nchini Marekani baadae mwaka huu, imekuwa nyeupe, baada ya hasimu wake mkuu Ted Cruz kujitoa katika kinyanganyiro.
 

Donald Trump, bilionea wa New York ambaye hakuwahi kushikilia wadhifa wowote wa umma amekuwa akiwaacha na mashangao magwiji wa kutabiri kwamba kampeni yake ingesambaratika.

Amekuwa akishinda licha ya kutoa matamshi ya kuchukiza katika kampeni zake, ambayo yamekosolewa vikali lakini bado yakaendelea kupamba harakati zake za kuupinga mfumo wa sasa.

Nyota huyo wa zamani wa vipindi vya uhalisia vya televisheni, sasa anajiandaa kwa mchuano wa uchaguzi wa Novemba 8, ambapo Hillary Clinton anatazamiwa kuwa mpinzani wake kutoka chama cha Democrat.

Trump ameitaja Indiana kuwa ni ushindi mkubwa na mara moja akanza kuelekeza mashambulizi dhidi ya Clinton. "Sasa tunamfuata Hillary Clinton. Hatokuwa rais mzuri, atakuwa rais mbaya, hajui biashara, mume wake alisaini makubaliano mabaya zaidi ya biashara katika historia, yanaitwa NAFTA," alisema Trump.


Hillary Clinton anatarajiwa kuchuana na Donald Trump katika uchaguzi mkuu wa Novemba 8, 2016.

Changamoto zinazomkabili

Changamoto ya sasa ya Trump ni kukiunganisha chama cha Republican, kwa sababu wanachama wengi watiifu wamekasirishwa na mtindo wake wa uonevu, udhalilishaji wa wanawake na mapendekezo yake ya kujenga ukuta kwenye mpaka na Mexico, na kuwafukuza wahamiaji haramu milioni 11.

Trump alitoa wito wa kuwepo na umoja katika hotuba yake ya ushindi, ambayo safari hii haikuwa na makeke na ushaufu vilivyozoeleka. Ushindi wake umefuta imani kwamba Warepublican wangemchagua mteule wao katika mkutano mkuu wa chama wakati viongozi watakapokutana mjini Cleveland Julai 18-21.

Anatazamiwa kukamilisha uteuzi rasmi Juni 7 wakati jimbo la California litakapopiga kura, ingawa gavana wa Ohio John Kasich ameapa kuendelea na kampeni kama mpinzani wa mwisho wa Trump.

Mwenyekit wa taifa wa chama cha Republican Reince Priebus amemtaja Trump kuwa mteule mtarajiwa wa chama katika matamshi aliyoyaweka kwenye ukurasa wake wa twita na kusema,"Sote tunahitaji kuungana na kuelekeza nguvu katika kumshinda Clinton.


Mrepublican Ted Cruz akiwapungia mashabiki wake baada ya kuamua kusitisha kampeni zake.

Mwisho wa matumaini

Wakati kura zikianza kutangazwa, Cruz mweye umri wa miaka 45 alitangaza kuwa anasitisha kampeni zake mjini Indianapolis, kwa sababu haoni tena njia ya kupata uteuzi.

"Tangia mwanzo nimesema nitaendelea maadamamu kuna njia inayoweza kutufikisha kwenye ushindi. Lakini usiku huu, nasikitika kusema kwamba inaonekana njia hiyo imefungwa," alisema Cruz, ambaye ni Seneta wa jimbo la Texas.

Cruz alikuwa akitegemea ushindi katika uchaguzi wa Jumanne kumsaidia kupunguza kasi ya Trump kuelekea uteuzi, lakini Trump aliendeleza kasi ya ushindi katika majimbo matano ya kaskazini-mashariki wiki iliyopita kuipokonya Indiana kutoka kwa Cruz, ambaye ukristo wake wa kihafidhina ulitarajiwa kumsaidia kushinda katika jimbo hilo.

Baadhi kwenye mkutano wake walishtushwa na uamuzi wa Cruz kujitoa kwenye mbio hizo. Dan Follis mwenye umri wa miaka 62, alitikiswa pia na tangazo la Cruz, lakini alikuwa ana uhakika wa jambo moja: "Sitomchaguwa Trump."

Kwa mujibu wa shirika la Associated Press, Trump alishinda wajumbe wasiopungua 51 kati ya 57 wanaotolewa kwa jimbo la Indiana. Ushindi huo umepelekea idadi ya wajumbe wake kufikia 1,047 kati ya jumla ya wajumbe 1,237 wanaohitajika kupata uteuzi, ikilinganishwa na wajumbe 153 alionao Kasich. Cruz alikuwa na wajumbe 565 kabla ya kusitisha kampeni zake.


Bernie Sanders ameshinda kura ya mchujo ya Indiana, lakini hana matumaini ya kumshinda Clinton.

Kambi ya Clinton yaanza mikakati

Kampeni ya Clinton iliashiria mkakati wake kumshughulikia Trump, katika taarifa iliyotolewa na mshauri mwandamizi wa Clinton John Podesta, ambae alisema Trump anataka kuwatisha na kuwagawa Wamarekani.

Alisema wakati wote wa kampeni zake, Donald Trump ameonesha kuwa mwenye kuwagawa raia na hana silika ya kuiongoza Marekani na ulimwengu huru, na kuogeza kuwa kumchagua itakuwa hatari kubwa zaidi kwa Marekani.

Tayari bibi Clinton amefikisha wajumbe 2,202 kati ya jumla ya wajumbe 2,383 wanaohitajika kushinda uteuzi wa chama cha Democratic, huku Bernie Sanders akiwa na wajumbe 1,400. Lakini Sanders amesema mapambano bado yanaendelea.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, dpae, ape.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post