TANESCO Yawataka Wateja wake Kuunganishiwa Umeme na Mafundi Waliosajiliwa ili Kupunguza Ajali za MotoShirika la Umeme Tanzania Nchini (TANESCO) limewataka wateja wake kuhakikisha wanaunganishiwa umeme na mafundi au wakandarasi waliosajiliwa na shirika hilo ili kupunguza ajali za moto.


Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Afya na Usalama kazini wa TANESCO, Mhandisi Majige Mabulla alipokua akiongea na waandishi wa habari juu ya vyanzo vya ajali za moto vinavyosababishwa na umeme.


Mhandisi Mabulla alisema kuwa matukio ya moto yanayosababishwa na umeme hutokea kutokana na kuzalishwa kwa joto kali ndani ya nyaya kunakosababishwa na umeme kuwa mkubwa kuliko uwezo, kulegea kwa maungio ya nyaya pamoja na radi au nyaya za umeme kuangukia juu ya paa la nyumba.


Kwa mujibu wa Mhandisi Mabulla aliongeza kuwa ajali za moto zinazosababishwa na umeme huanza kama unavyoanza moto wa kiberiti au viwashio vinginevyo vya moto na husambaa haraka kwa kutegemea na aina ya vitu vilivyopo kwenye eneo husika kwa kuwa baadhi ya vitu hushika moto haraka na kuenea kwa kasi.


“Ajali za moto zinazosababishwa na umeme ni ngumu kutokea kama umeme utasukwa na mtaalam aliyebobea kwenye fani hiyo, TANESCO tunatoa wito kwa wateja wetu kuhakikisha wanafungiwa umeme na fundi au mkandarasi aliyesajiliwa na kampuni yetu,”alisema Mabulla.


Pia Mhandisi Mabulla alisema ili kuepukana na ajali za moto zinazotokana na hitilafu za umeme wateja wanapaswa ;kuepuka kupitisha nyaya za umeme juu ya paa za nyumba, kutokuunganisha umeme kutoka nyumba moja kwenda nyingine bila kupata maelekeza kutoka TANESCO.


Aidha Mhandisi Mabula alisema wateja pia wanapaswa kuhakikisha mfumo wa umeme unapitiwa upya kila baada ya miaka mitano pamoja na kuwa makini katika utumiaji wa vifaa vinavyotumia umeme kama vile pasi, hita za umeme.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post