Songas Yazima Mitambo Yao kwa Kuidai Tanesco Sh Blioni 194

Kampuni ya kufua umeme kwa njia ya gesi asilia, Songas Limited imezima mitambo yake, baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushindwa kulipa deni la Dola 90 milioni za Marekani sawa na Sh193.5 bilioni, jambo linalotishia ukosefu wa nishati hiyo muhimu nchini.


Hata hivyo, Tanesco imepinga uamuzi huo na kueleza kuwa ni vitisho kwa wananchi na inakiuka vifungu namba 4.4 , 4.6 na 17 vya mkataba ulioingiwa na Songas.

Mkurugenzi Mkuu wa Songas, Nigel Whittaker alisema jana kuwa wameamua kuchukua hatua ya kuzima mitambo hiyo baada ya kuzidiwa na gharama za uendeshaji kutokana na deni hilo.


“Mtambo huo uliopo Ubungo unazalisha Megawati 189, tumefikia hatua ya kuzima kidogo kidogo kuanzia Aprili 29 mwaka huu kutokana na deni hilo, Tanesco imekuwa ikisuasua katika kulipa,” alisema Whittaker.


Alisisitiza kuwa mradi huo wa Songas, ulioanzishwa tangu mwaka 2004 , ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na umekuwa ukizalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kutoka Songosongo na kuuingiza katika gridi ya taifa.


Whittaker alieleza kuwa kiasi cha umeme wanaozalisha ni takriban asilimia 20 ya nishati inayozalishwa nchini.


“Ilikuwa tuifunge mitambo hii tangu mwaka jana, lakini Serikali ilituomba tuendelee wakati ikisimamia hatua ya kulipwa, tunaendelea lakini hatimaye tumekwama kwa kuwa kuna mahitaji ya msingi ambayo yanategemea fedha ikiwamo matengenezo ya mitambo hiyo,”alisema.


Alisema pia wamejikuta katika hali ngumu kwa kudaiwa na taasisi kadhaa za Serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), hivyo wanaendelea kujadiliana na Tanesco na Serikali ili kuangalia jinsi ya kushughulikia jambo hilo kwa kutambua umuhimu wa mradi huo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alisema Songas wamevunja makubaliano ya mkataba hususan kifungu cha 4.4 ambacho kinaitaka Songas kutoa siku 90 ya kuwa na majadiliano.


Aliwatoa wananchi hofu kwa nchi haitaingia gizani kwa kuwa licha ya Songas kutangaza kuzima kabisa mitambo yote Mei 11.

"Tayari walikwisha kuwa wameanza kuizima na haututokea mgawo. Ingawa ni kweli wanatudai, lakini siwezi kusema kiasi gani nami nitakuwa nimekiuka huo mkataba, kwa hili walilofanya tutachukua hatua hatukubaliani nao,” alisema.


Songas ambao taarifa ya hivi karibuni ya Serikali inaonyesha kuwa wanauzia umeme Tanesco kwa senti za 2.4 za Marekani kwa uniti, wanalipwa capacity charge ya Dola za Marekani 5.2 milioni kwa mwezi ambazo ni sawa na wastani wa Sh11.4 bilioni.


Kulingana na hesabu hizo, kila mwaka kampuni hiyo inalipwa Sh136.9 bilioni tangu 2001 walivyoingia mkataba na Tanesco.


Mahitaji makubwa ya umeme Tanzania mara ya mwisho yalirekodiwa kuwa megawati 898.5.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post