Polisi Yaua Majambazi Wanne Katika Mapango ya Amboni Tanga

Watu wanne wameuawa katika mapambano na polisi yaliyotokea kwenye mapango ya Amboni mjini Tamga, eneo ambalo polisi mmoja aliuawa Februari mwaka jana katika tukio lililohusishwa na ugaidi.


Katika tukio hilo la Februari mwaka jana, polisi walilazimika kuomba msaada wa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kukabiliana na watu waliokuwa wamejificha kwenye mapango hayo na kupiga kambi hapo hadi walipokisambaratisha kikundi hicho kilichoelezwa kuwa na sura ya ugaidi.


Mapambano ya jana yametokea kwenye eneo hilo la kihistoria wakati polisi wakiendesha operesheni ya kusaka majambazi waliofanya mauaji katika duka la Central Bakery.


Majambazi hao walivamia duka maarufu la Central Bakery mwezi uliopita na kuwaua watu wanne, kujeruhi wawili na kupora Sh2.7 milioni baada ya kufanikiwa kuvunja kasiki.


Jana ilikuwa siku ya tatu tangu milio ya risasi ianze kusikika katika mapango ya Amboni na baadaye taarifa kuenea jijini Tanga kuwa kulikuwa na majibizano ya risasi.


Kamanda wa polisi wa mkoa, Leonard Paulo aliwataja waliouawa katika mashambulizi ya risasi yaliyotokea katika mapango ya Amboni kuwa ni Nasibu Bakari, Abuu Katada, Abuu Mussa na raia wa kigeni aliyetambulika kwa jina la Idrisa Berato.


Kamanda Leonard alisema mbali na kuwathibiti majambazi hao, pia jeshi hilo limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vinavyosadikika kuwa vilikuwa vinatumika katika matukio ya ujambazi.


Alivitaja vifaa vilivyokamatwa kuwa ni vocha mbalimbali za simu 195, majambia saba, mapanga manne, msumeno mmoja, risasi 17 za shortgun, sare za mgambo, kofia inayofanana na ya sare za JWTZ na pikipiki mbili.


Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi, watu wanne walikamatwa na waliwataja wenzao ambao walijificha kwenye mapango hayo na ndipo jeshi likavamia eneo hilo na kufanikiwa kuua watu wanne na kujeruhi mmoja.


Alisema Katika majibizano ya risasi, askari wawili walijeruhiwa, akiwataja kuwa ni Gwantwa Mwakisole, mkaguzi msaidizi wa polisi mkoani Tanga na PC Charles.


Habari zinaarifu kuwa viongozi waandamizi wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu wako jijini Tanga tangu kutokea kwa mauaji hayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post