WAZIRI MKUU MSTAAFU WA KENYA RAILA ODINGA AAGANA NA RAIS MAGUFULI KIJIJINI KWAKE


Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Amolo Odinga amerejea nchini Kenya baada ya kumaliza mapumziko yake ya siku tatu huko Lubambangwe katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, alikomtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyepo mapumzikoni.


Akizungumza katika uwanja wa michezo wa shule ya Sekondari ya Chato kabla ya kuruka kwa Helkopta, Mheshimiwa Odinga amemshukuru rafiki yake Rais Magufuli kwa kumpokea na pia amewashukuru wananchi wa Chato kwa ukarimu wao kwa wageni.


Mheshimiwa Odinga pia amesema ana imani kuwa Rais Magufuli ataisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo umasikini unawakabili wananchi wake.


"Lakini mimi najua yeye mwenyewe ana maono, anaona mbele na anajua yale ambayo yanatakiwa yafanyike ili Tanzania iinuke, itoke katika hali ya ufukara na kuwa katika hali ya maendeleo zaidi" Amesema Mheshimiwa Odinga.


Mheshimiwa Raila Amolo Odinga na Mkewe Mama Ida Odinga waliwasili Chato tarehe 02 April, 2016 kwa mapumziko na kuisalimia familia ya Rais Magufuli ambayo ni familia rafiki.


Katika Hatua nyingine Rais Magufuli ameahidi kutoa madawati na vitabu kwa wanafunzi wa shule tatu za Msingi zilizopo Chato, ambao walijitokeza katika uwanja wa Sekondari wa Chato, wakati Rais Magufuli akimuaga mgeni wake Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Raila Odinga.


Shule hizo ni Chato, Kalema na Kitela.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato
04 April, 2016





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post