WATUHUMIWA WA TUMBILI WASAKA DHAMANA MAHAKAMA KUU
Raia wawili wa Uholanzi na vigogo wanne wa Wizara ya Maliasili na Utalii wanaoshtakiwa kwa kutaka kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Armenia, wamewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.


Washtakiwa hao waliofikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Aprili Mosi, walirudishwa mahabusu na kutakiwa kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu.


Sheria ya Uhalifu wa Kupangwa ikisomwa na kifungu 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya 2002, inataka kesi ya uhujumu uchumi kwa kosa linalozidi Sh10 milioni isikilizwe na Mahakama Kuu.


Habari zilizothibitishwa na uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana zilieleza kwa nyakati tofauti mawakili wa utetezi kutokea jijini Arusha waliwasilisha maombi hayo juzi.


Waholanzi hao, Artem Vardanyian (52) na Eduard Vardanyian (46) na Mtanzania Iddy Misanya ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Arusha Birds Traders wamefungua maombi namba 3/2016.


Washtakiwa wengine, Dk Charles Mulokozi amefungua maombi namba 5/2016 wakati Nyangabo Musika (39), Martina Nyakangara (34) na Very Anthony (33) wamefungua maombi namba 4/2016.


Dk Mulokozi ni Naibu Mkurugenzi wa Wanyamapori (Rasilimali Endelevu), Nyakangara, Martina na Very ni maofisa wa Idara ya Wanyamapori.


Mawakili wa utetezi, Robert Rogath, John Masangwa na Alex Artem ambaye ni mtoto wa Artem, walionekana siku nzima juzi na jana nje ya viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi wakifuatilia maombi hayo.


Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Bernard Mpepo alithibitisha kupokelewa kwa maombi hayo na kwamba, yapo mezani kwa Jaji Mfawidhi, Aishiel Sumari kwa hatua zaidi za kisheria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post