Ofisi ya Elimu wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani imelazimika kuwapa likizo walimu saba wa Shule ya Msingi Mingwata ili kuwajenga kisaikolojia baada ya kukithiri kwa matukio ya kishirikina yanayowakumba katika shule hiyo.
Walimu hao wanakumbana na matukio ya ajabu ikiwamo kujikuta uchi, kupigwa fimbo na mtu asiyeonekana na kulazwa nje ya nyumba zao.
Mmoja wa walimu walioathirika na matukio hayo, Emmanuel Shaaban alisema yeye na familia yake hawana raha kutokana na matukio hayo kwa kuwa usiku huvuliwa nguo na kujikuta wamelazwa sehemu nyingine, huku wakiwa wamechanjwa kwa wembe mwili mzima.
“Tarehe 26 mwezi wa pili, siku ya Alhamisi sitaisahau kabisa. Ndiyo siku ambayo nilikatwa viwembe mwili mzima na hali yangu ilikuwa mbaya, niliishiwa nguvu na mwili ukawa na ganzi na nilipokwenda hospitali niliambiwa sina ugonjwa,” alisema Shaaban.
Alisema alipotoka hospitali alikwenda kijijini kwao mkoani Mwanza na huko aliendelea kuwa na hali mbaya kutokana na kuzimia mara kwa mara kwa sababu ya maumivu ya kichwa hadi alipotibiwa kienyeji.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mikidadi Mbelwa alisema awali alikuwa akiona vituko usiku na mchana, lakini alivumilia huku akitunza siri bila kuwaeleza wenzake ili asiwakatishe tamaa.
Mbelwa alisema baadhi ya matukio aliyokutana nayo ni kuvuliwa nguo usiku, kulazwa eneo jingine, kuchapwa viboko, kumwagiwa damu kwenye korido ya nyumba, kuchanjwa kwa wembe, kuzungukwa na nyoka mwilini, kuona mtu na kisha anapotea na kutupwa kwenye mashimo.
Mzazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo, Asha Kondo alikiri kuwapo kwa matukio ya watoto kuugua na kuanguka hadi uongozi wa kijiji ulipopeleka mganga wa kienyeji kutoa kinachodaiwa ni uchawi.
Mratibu wa Elimu wa Kata ya Marui, Damaru Charles alisema amekuwa akipokea malalamiko hayo na kuyawasilisha ngazi za juu.
Ofisa Elimu Msingi wilayani hapa, Aurelia Rwenza alisema tatizo hilo linawapa shida walimu na kurudisha nyuma maendeleo ya elimu katika sehemu hiyo.
“Kwa kweli walimu wameathirika, hivi sasa tunatakiwa kuwajenga kisaikolojia,” alisema.