TB Joshua Atajwa Kashfa ya Ukwepaji Kodi ya Panama,Mwenyewe Afunguka Mazito

 
TB Joshua, muhubiri maarufu barani Afrika na raia wa Nigeria, ametajwa kwenye nyaraka za kashfa ya ukwepaji kodi za Panama, akidaiwa kuwa na hisa kwenye kampuni iliyosajiliwa visiwa vya British Virgin Islands.

Mwanzilishi huyo wa Kanisa la Sinagogi la Mataifa Yote (Synagogue Church of All Nations) na mkewe Evelyn wanadaiwa kuwa na hisa kwenye kampuni hewa ya Chillon Consultancy Limited iliyo kisiwa cha Tortola, ambacho ni kikubwa kuliko vyote vya British Virgin na ambacho hakuna watu wengi wanaoishi.

Wote wawili wanamiliki hisa moja, ingawa kampuni hiyo yenye namba ya usajili 1033675, inaidhinishwa kutoa hisa zisizozidi “50,000 kwa thamani ya hisa ya daraja moja.” Haieleweki ni biashara gani TB Joshua alifanya na kampuni hiyo ambayo haina ofisi kwenye kisiwa hicho cha Tortola.

Lakini muhubiri huyo, ambaye alifuatwa na wagombea wawili wa urais wa Tanzania, John Magufuli na Edward Lowassa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, amekanusha vikali tuhuma hizo zilizoandikwa na gazeti la Premium Times la Nigeria, akisema zina lengo la kumchafua yeye na kanisa lake na kwamba aliyeandika habari hiyo, Nicolas Ibekwe aliwahi kumtuhumu kuwa alimpa rushwa wakati jengo la nyumba ya wageni la kanisa lake lilipoanguka.


“Mimi si mfanyabiashara na sina biashara. Kitu alichonipa Mungu si cha kawaida. Sihusiki na nyaraka za Panama,” alisema TB Joshua katika taarifa yake aliyoituma kwenye ukurasa wa facebook.
“Mimi na familia yangu tutaendelea kuwa kwenye shamba la Mungu. Premium Times – msiruhusu kampuni yenu kutumika. Msiruhusu kampuni yenu kupingana na Mungu. “Huu ni uongo! Zingatia – habari hii imeandikwa na mwandishi yule yule ambaye alinituhumu kuwa nilimuhonga wakati wa tukio la jengo kuanguka na alienda kwenye vyombo tofauti vya habari – vya ndani na vya kimataifa – kutangaza mambo hayo ya kutunga.


“Tangu wakati wa tukio la jengo, kumekuwa na mfululizo wa vitisho dhidi ya huduma yangu na mimi binafsi kutoka kwa mwandishi huyo, Nicholas Ibekwe, ambaye anawakilisha kikundi cha watu.”
Alisema: “Baada ya yote hayo yaliyofanywa kujaribu kuimaliza huduma hii, hiki ndicho alichoamua kukifanya. Hata picha iliyotumika kwenye habari ilipigwa kwenye mkutano wa injili nilioufanya Mexico. Nilikwenda kwenye mkutano wa injili, na si vinginevyo.”

Muhubiri huyo alitaka nyaraka za Panama zisitumike kushambulia watu ambao wamekuwa wakiwatafuta ili wawachafue kwa kuwa si kila mtu anayetuhumiwa na vyombo vya habari kuhusika kwenye sakata hilo, amehusika.


“Suala langu ni mfano mzuri,” alisema. TB Joshua amejizolea umaarufu kutokana na kutabiria watu matukio yanayotarajiwa kuwatokea na amekuwa akivuta waumini kutoka kila kona ya Afrika kwenda Nigeria kumsikiliza.
Kwa nyakati tofauti, Magufuli wakati akiwa waziri, na Lowassa walikwenda Nigeria kuhudhuria mahubiri yake na taarifa zinasema kuwa wote walitabiriwa urais.

Wawili wao walichangia kuufanya uchaguzi mkuu uliopita kuwa na msisimko na ushindani mkali, kabla ya Magufuli kuibuka mshindi kwa kupata kura milioni 8.8, akifuatiwa na Lowassa aliyepata kura milioni 6.07. Baada ya Uchaguzi Mkuu, TB Joshua alikuja nchini na kufanya mazungumzo na Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na baadaye kutumia muda uliosalia kwa kuwa karibu na Lowassa kabla ya kurudi Nigeria. Nyaraka hizo zilivuja kutoka kampuni ya sheria ya Mossack Fonseca ya Panama iliyokuwa ikisaidia wanasiasa, wafanyabiashara na watu maarufu duniani kusajili kampuni hizo.

Nyaraka za Panama zimefichua watu maarufu 143 duniani wakiwamo wakuu 12 wa nchi walioko madarakani na waliostaafu pamoja na familia zao na marafiki wa karibu ambao wamenufaika na ukwepaji kodi. Miongoni mwao ni baba wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Davi Cameron, hayati Ian Cameron ambaye inadaiwa kila alipokuwa anakwenda kuhudhuria kikao cha bodi cha kampuni ya Blairmore Holdings, alianzia kwenda Uswisi au Bahamas.

Awali David Cameroon alikana kuhusika katika kashfa hiyo lakini juzi alikiri kumiliki hisa katika kampuni ya baba yake ambayo iliuzwa kabla hajawa Waziri Mkuu.

Wengine ni Sergei Roldugin, mshirika wa Rais Vladimir Putin wa Russia, shemeji wa Rais Xi Jinping wa China, Rais Mauricio Macri wa Argentina, na watoto watatu wa Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif.

Pia yumo Ahmad Ali al-Mirghani, rais wa zamani wa Sudan, Kalpana Rawal (Naibu Jaji Mkuu wa Kenya), Koffi Annan (katibu mkuu wa zamani Umoja wa Mataifa), Mounir Majid (msaidizi wa karibu wa Mfalme wa Morocco) na Khulubuse Zuma (mpwa wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post