Ushirikina Shinyanga!! Nyumba Saba Zamwagiwa Damu,Dumu na Kitambaa Chenye Maandishi ya Damu Vyazua Taharuki ( Picha)Watu wasiojulikana wamemwaga damu kwenye milango ya familia saba huku nyumba ya nane ikipewa vitisho kwa maandishi ya rangi nyekundu yanayodaiwa kuwa ni ya damu kwenye kitambaa cheupe na kwenye dumu lenye ujazo wa lita tano likiwa na mafuta yanayodaiwa kuwa ya petroli katika mtaa wa Mageuzi kata ya Ngokolo mjini Shinyanga.


Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 12 asubuhi baada ya familia hizo kuanza kuamka na kukuta damu isiyojulikana ni ya mnyama gani ikiwa imetapakaa kwenye milango ya familia hizo na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo hilo waliofika eneo hilo.

Tukio la kumwagwa damu katika familia hizo limezua hofu kwa wakazi wa eneo hilo huku wengi wakilihusisha na imani za kishirikina na wengine kudai kuwa pengine ni vitisho tu vya vijana wa mtaani.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema tukio la kumwagwa damu kwenye milango yao linaashiria dalili mbaya hivyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.

“Usiku tumesikia sauti za mbwa na paka wakilia sana,hatukujua nini kinaendelea asubuhi hii ndiyo tumekutana na majanga haya,familia zetu zimemwagiwa damu kwenye milango,hatujajua ni damu ya mnyama gani,lakini tukio hili siyo la kawaida na halijawahi kutokea”,walisikika wakisema wakazi wa eneo hilo.

Akisimulia kuhusu tukio hilo mmoja wa wamiliki wa nyumba hizo Mussa Massaba,ambaye nyumba yake ipo katikati ya nyumba zilizopakwa damu na ndipo kumekutwa damu nyingi, alisema familia yake imeingiwa na hofu kwani haijulikani watu walioweka damu hiyo wana malengo gani.

“Nimeamka saa 12 na nusu asubuhi kuzima taa ya nje,nikakuta damu mbichi mlangoni kwangu,nikawaamsha wapangaji wangu kisha kutoa taarifa kwa viongozi wa mtaa waliofika hapa,lakini kumbe tukio halikuwa kwangu tu,hizi nyumba za jirani nazo kuna damu kwenye milango yao ila kwangu ndiyo nyingi zaidi”,alieleza Massaba.

“Usiku hatukusikia sauti ya mtu yeyote akigonga mlango wala kusikia akitembea,badala yake kulikuwa na sauti za mbwa na paka wakilia,hatujaona hata unyayo wa mtu hapa nje,tunaomba serikali kuchunguza suala hili kwani sasa usalama wetu ni mdogo,hii ni dalili ya hatari ,tunachofanya sasa ni maombi tu”,aliongeza Masaba.

Naye Magdalena Allex ambaye pia nyumba yake imemwagiwa damu mlangoni alisema kilichofanyika ni mchezo wa kishirikina na kwamba,tunaomba waliofanya kitendo hiki waache kwani havina faida yoyote kwa jamii.

“Mtu unashindwa kulala kwako usiku na kuanza kuwanga kwenye nyumba za watu,naomba jamii iachane na mambo haya kwani wanatishia amani kwenye familia zetu na mtaa kwa ujumla”,alieleza Allex.

Mbali na familia hizo saba kumwagiwa damu pia,nyumba moja katika mtaa huo imetishiwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana waliodai kuwa wanamdai mmiliki wa nyumba hiyo kiasi cha shilingi milioni 11 alizowadhurumu.

Katika nyumba hiyo inayomilikiwa na Hamis Reli Mathayo na mke wake Loyce Busumba Gigo kumekutwa na dumu la lita tano likiwa na mafuta ya petrol na kitambaa cheupe vyote vikiwa na maandishi mekundu ya vitisho kuwa watachoma nyumba hiyo kwa madai kuwa wameshurumiwa.

“Wizi wako umeiba kwa watu wasioibiwa,tumekupa wiki moja uje utoe maelekezo unayowadanganya wengine tunaofanya nao kazi …tumekupa siku mbili uje na pesa zote milioni 11 ulizoiba,kama hauji nyumba hii iteketezwe kwa moto..sasa kazi imeanza utakuta nyumbani kwako..wewe ni mwanamke tu huwezi kuibia wanaume”,ulisomeka ujumbe ulioandikwa kwa maandishi mekundu katika dumu na kitambaa hicho cheupe.

Mmoja wa watoto wa familia hiyo Mariam Hamis( 20) alisema walipoamka asubuhi walikuta dumu hilo likiwa na maandishi mekundu na kitambaa cheupe kikiwa na maandishi mekundu ya vitisho vya kuchomewa nyumba yao.

“Baba yuko kikazi huko Salawe Shinyanga vijijini,mama naye yupo kwenye msiba huko Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga,mara nyingi baba huwa haji nyumbani ana familia nyingine huko Salawe tumempigia simu kuhusu tukio hili anasema tumwambie mama ambaye naye yuko msibani ndipo tukaamua kutoa taarifa kwa viongozi wa mtaa”,alisema Hamis.

“Hili tukio limetushtua,sasa tunaishi kwa hofu kubwa,tunaomba uongozi wa mtaa na jeshi la polisi watusaidia kuimarisha ulinzi hapa nyumbani,hatujui wazazi wetu wamefanya nini hadi tuchomewe nyumba”,aliongeza motto huyo.

Akizungumzia juu ya matukio hayo, mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Emmanuel Joshua aliyekuwa eneo la tukio aliiambia Malunde1 blog kuwa  uongozi wa mtaa huo kwa kushirikiana na jeshi la polisi na wananchi wa mtaa huo wanaendelea kufanya uchunguzi wa matukio hayo na kwamba watachukua hatua kali kwa wataobanika kuhusika na vitendo hivyo.

“Haya matukio yamewatia hofu wakazi wa eneo hili,tunaomba wananchi wasiyahusishe na imani za kishirikina kwani pengine kuna watu walifanya uhalifu na kupita maeneo ya familia hizi wakiwa wanavuja damu,tunaomba tushirikiane kuwafichua wahusika wa matukio haya”,aliongeza Joshua.

Hata hivyo mmoja wa maafisa wa jeshi la polisi aliyekuwa eneo la tukio aliyedai kuwa yeye msemaji wa jeshi la polisi aliwasihi wananchi kuwa watulivu na kutohusisha tukio la umwagaji damu na ushirikina huku akiondoka na kitambaa na dumu la mafuta ya petroli lililokutwa kwenye familia ya Hamis Reli Mathayo. 


Akizungumza na Malunde1 blog kwa njia ya simu,Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Dismas Kisusi alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi aliyekuwepo eneo la tukio,alisema bado hajapokea taarifa kuhusu matukio hayo na kuahidi kutoa taarifa kuhusu matukio hayo mara tu atakapopelekewa taarifa.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Angalia picha hapa chini


Matone ya damu yakiwa katika sakafu karibu na milango ya nyumba ya Mussa Masaba katika mtaa wa Mageuza katika manispaa ya ShinyangaMatone ya damu yakiwa sakafuni


Matone ya damu yakiwa kwenye mlango wa nyumba ya Mussa Masaba
 
Sakafu ikiwa na damu


Wakazi wa mtaa wa Mageuzi wakishangaa damu kwenye moja ya nyumba hizo 7Wananchi wakiwa katika moja ya nyumba zilizomwagiwa damu
Kushoto ni mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel Joshua akimwonesha damu mwandishi wa habari wa Radio Faraja Fm Stereo na DW Veronica NatalisMwandishi wa habari Veronica Natalis akifanya mahojiano na mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel JoshuaMwandishi wa habari akizungumza na familia ya Mussa Masaba ambapo ndipo damu nyingi imemwagwaMagdalena Allex akionesha damu katika mlango wa nyumba yake
Mwandishi wa habari Veronica Natalis akifanya mahojiano na Magdalena AllexBaadhi ya nyumba zilizomwagiwa damu kwenye milango

Dumu la mafuta na kitambaa cheupe vikiwa katika nyumba ya Hamis Reli Mathayo katika mtaa wa Mageuzi
Kitambaa kikiwa na maandishi mekundu ya vitisho katika nyumba ya Hamis Reli MathayoDumu likiwa na maandishi ya vitishoDumu likiwa na maandishi ya vitisho
Dumu likiwa na maandishi kila upandeDumu la mafuta
Kitambaa kikiwa na maandishi ya vitishoWananchi wakiwa nje ya nyumba ya Hamis Reli MathayoNyumba ya Hamis Reli Mathayo inayotaka kuteketezwa kwa moto kama hatarudisha pesa anazodaiwa

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post