RAIS MAGUFULI ATISHIWA KUUAWA KWA KUJITOA MHANGA
Kondakta wa daladala, Hamim Seif (42) mkazi wa Mwananyamala Ujiji, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kutishia kumuua Rais John Magufuli kwa maneno.


Seif alipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana mchana na kusomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kenneth Sekwao.


Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo na Hakimu Mkazi, Hellen Liwa alisema kuwa dhamana ya mshtakiwa huyo iko wazi na alitakiwa kuwa na wadhamini wawili, kutoka taasisi ya Serikali inayotambulika, ambaye atasaini hati ya dhamana ya Sh2 milioni.


Licha ya dhamana yake hiyo kuwa wazi, mshtakiwa huyo alishindwa kukamilisha masharti hayo kwani baada ya kusomewa mashtaka alipoulizwa kama alikuwa na wadhamini alishindwa kuwapata.


Akimsomea shtaka linalomkabili, Wakili Sekwao alisema kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 10 mwaka huu katika baa ya Soweto, Makumbusho wilayani Kinondoni kinyume cha kifungu cha 89 (2) (a) na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.


Wakili Sekwao alisema akiwa katika baa hiyo, mshtakiwa alitishia kumuua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli kwa maneno kwa njia ya kujitoa mhanga.


“Kwa haya mambo anayoyafanya Rais Magufuli, mimi nimo tayari kujilipua kwa kujitoa mhanga ili kumuangamiza,” alisema Wakili Sekwao akimnukuu mshtakiwa huyo.


Hata hivyo, Wakili Sekwao alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post