Rais Magufuli Ampaisha Dr. Ramadhani Dau wa NSSF Darajani


"Kabla sijaanza kuhutubia, naomba nimkaribishe mtu muhimu sana aliyefanikisha ujenzi wa Daraja hili. Dkt Dau tafadhali karibu usalimie kidogo’’. 
 
Ndivyo alivyoanza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli jana wakati wa uzinduzi wa daraja la kihistoria la kigamboni alilopendekeza liitwe daraja la Nyerere kutukuza mchango wa mwasisi wa taifa hili baba wa taifa hayati mwalimu Julius kambarage nyerere.

"Watanzania wana tabia ya kusahau sana. Tunaweza kuzindua hapa wakashangilia lakini wasiwapongeze watu waliofanikisha kazi hiyo..mnyonge mnyongeni haki yake mpeni”. Aliendelea Rais Magufuli mara baada ya Dk. Dau kumaliza kusalimia.

Dk Magufuli alisema Balozi Dau alimfuata ofisini kwake(wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi), akiwa mnyonge na mwenye kukata tamaa ya kufanikisha mradi huo.

“Ndiyo nikamwambia aanze kufanya kazi.” Rais Magufuli alisema ni Dk Dau na NSSF ndiyo waliosimamia na kuhakikisha daraja hilo linajengwa na kukamilika kwa kiwango hicho, akasema haitakuwa busara kulizindua bila kutambua mchango wake.

Alisema ni kawaida kwa watu wenye michango mikubwa kusahaulika wakati wa mafanikio.

Tukio hilo lilionyesha dhahiri kwamba Rais Magufuli amevutiwa kwa kiasi kikubwa na kazi ya mkurugenzi huyo mstaafu wa NSSF na kwenda tofauti na matarajio ya watu wengi waliokuwa na shauku ya kumsikia Rais akimchukulia hatua mkurugenzi huyo kwa madai ya ubadhirifu wa mabilioni ya fedha .

Hatua hii ya Rais kumwagia sifa hadharani Dk. Dau, inakuja siku chache baada ya kusambazwa kwa kinachoitwa taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali CAG taarifa ambazo baadae zilikanushwa na ofisi ya CAG .

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Dau alizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa NSSF katika uwekezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Aliwakumbusha Watanzania kumtanguliza Mungu akisema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kukuza uchumi na kurahisisha usafirishaji kwa wakazi wa Kigamboni na Tanzania kwa ujumla.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema daraja hilo ni la kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwamba litasaidia kukuza uchumi, utalii na ndiyo maana hata majirani wanalitamani.

“Daraja hili linabeba zaidi ya tani elfu moja, ni daraja la kipekee, linao uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 100,” alisema .

Alisema katika ujenzi wake uliofanyika kwa utaratibu wa PPP (Public Private Partnership), Serikali imetoa asilimia 40 na NSSF asilimia 60 hivyo vyombo vya usafiri kama baiskeli, guta, pikipiki na magari yatalipa kuvuka.

“Leo hii, daraja hili limekamilika... halitambagua mtu kwa sababu wa CCM watapita hapa wa Chadema watapita hapa na bahati nzuri mstahiki meya wa jiji hili ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita katika daraja hili… lakini wananchi waenda kwa miguu hawatalipia matumizi ya daraja… ila wale waendesha baiskeli, pikipiki, maguta na magari lazima walipie,” alisema Dk Magufuli.

Rais aliipongeza kampuni ya China Railway Construction Engineering Group iliyotekeleza mradi huo kwa kushirikiana na kampuni ya China Railway Major Bridge Group.

“Kwa kazi nzuri iliyofanywa na wenzetu hawa kutoka nchini China napenda kutumia fursa hii kuahidi kwa niaba ya Serikali kuwa tutaendeleza ushirikiano wetu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo kumalizia kipande cha barabara kinachounganisha daraja hili kutoka upande wa Kigamboni,’’ alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post