OFISI YA WAKILI WA KUJITEGEMEA YALIPULIWA KWA BOMU HUKO ZANZIBAR

Watu wasiofahamika wamelipua kwa kitu kinachohisiwa kuwa ni bomu Ofisi ya Wakili wa Kujitegemea, Omar Said Shabani, iliyopo Kiembe Samaki Zanzibar.


Tukio hilo lilitokea saa 7:00 usiku wa kuamkia jana. Hata hivyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana na mlipuko huo isipokuwa jengo la ofisi hiyo limeharibika katika baadhi ya maeneo ikiwamo kuvunjika kwa vioo vya madirisha.


“Majira ya saa saba usiku, nilipata taarifa kuwa mlipuko umetokea katika ofisi yangu na nilipofika nilikuta mipasuko kidogo ya vioo vya nyumba yangu," alisema Wakili Omar.


Omar, ambae pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, alisema gharama za uharibifu wa mali hiyo bado hajazijua.


Aidha, alisema analiachia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wake.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kutokea kwa mlipuko huo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini aina ya bomu lililotumika.


Alisema taarifa kamili kuhusu mlipuko huo, atautoa baadaye kwa vile polisi wanaedelea na uchunguzi.


Aidha, Kamanda Mkadam aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu na kutoa taarifa ya vitendo vyote vinavyoashiria uhalifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post