MSD Yaigeuzia Kibao Muhimbili Kuhusu Kuhusu Utata wa Dawa Uliobuliwa na CAG


Sakata la upotevu wa vifaatiba na dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD) kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kipindi cha miaka minne limeingia katika sura mpya baada ya MSD kuigeuzia kibao hospitali hiyo, huku ikitoa ushahidi wa ankara 23 zilizotumika kupelekea vifaa hivyo kwa kipindi cha miaka minne.


Ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad inaonyesha ukaguzi ulifanyika Muhimbili, huku rekodi zikionyesha kwamba hospitali hiyo ilikuwa ikiagiza mzigo kutoka MSD, lakini hazionyeshi kupokea vifaa hivyo tangu mwaka 2012/14.


Kwa kutumia vielelezo vya nyaraka hizo mbele ya vyombo vya habari jana, MSD ilitoa ufafanuzi kuwa haihusiki katika upotevu huo kwani iliwasilisha MNH vifaatiba na dawa zenye thamani ya Sh2.6 bilioni na kupokewa stoo kwa nyakati tofauti kwa kipindi cha miaka minne.


Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Lauren Bwanakunu alisema hati za CAG, zinaonyesha kuwa MSD haina tatizo lolote.

“Ankara hizo siyo kwamba dawa hazikufika hospitalini hapo, bali hazikuonekana kwenye vitabu vya kupokelea mali vya Hospitali ya Taifa Muhimbili,” alisema.


Alisema baada ya kupitia nyaraka zake, MSD imefanikiwa kupata uthibitisho wa hati za kupelekea mali za dawa na vifaatiba vyote vilivyopelekwa Muhimbili, ambavyo ni pamoja na dawa za figo na moyo.

Bwanakunu alisema pamoja na juhudi hizo, Bohari ya Dawa imewasiliana na Muhimbili ili kuainisha taarifa za kwenye ankara na shehena ya dawa na vifaatiba vilivyopelekwa hospitalini hapo, kwani utaratibu wa kupeleka na kukabidhi dawa hospitalini unamlazimu mpokeaji kusaini ankara inayoonyesha mzigo uliopelekwa kwa mteja (delivery notes) ambazo zote zipo Bohari ya Dawa.


“Vitabu vyetu kutoka kwa CAG vipo na tumepata hati safi, tumethibitisha kwamba mzigo wote wa ankara 23 ulipelekwa Muhimbili kwa kipindi cha miaka minne,” alisema.


Alisema MSD ilikuwa ikiwasilisha dawa tangu mwaka 2012 kwa mujibu wa maombi kutoka MNH, hivyo hospitali hiyo inapaswa kujibu kwa kuwa imekuwa ikipokea dawa hizo kwa kipindi tofauti.

“Vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh2.03 bilioni vilikuwa vikiagizwa kwa tarehe tofauti kwa miaka mitatu lakini havikuwahi kuingizwa katika rekodi.


"Kulingana na utaratibu wa usambazaji wa MSD, mteja hukiri kupokea mzigo kupitia Ankara ya mauzo (Sales Invoice), jukumu la kuandika hati ya mapokeo (GRN) ni la mteja husika ambaye ni Muhimbili,” alisema Bwanakunu huku akionyesha nakala hizo.


Ankara zilizotolewa jana na MSD zinaonyesha kuwa ilikuwa ikihudumia hospitali hiyo tangu Mei 14, 2012 hadi Desemba 4, 2014, lakini katika ankara hiyo, Muhimbili haikuonyesha kuwahi kupokea vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh2,028,625,100.


Alichosema CAG
Katika ukurasa wa 37, taarifa ya CAG, inaeleza kuwa ukaguzi huo ulibaini kuwa dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh2.03 bilioni havijafika Muhimbili tangu Mei 2012 licha ya kuonekana kwenye ankara 23 za MSD.

Nakala hiyo ilieleza kuwa kwa hali ya kawaida, haikutarajiwa bidhaa hizo kuchukua zaidi ya wiki moja kufikishwa sehemu husika ukizingatia ofisi za MSD na MNH zote zipo Dar es Salaam.

“Hali hii inaashiria uwezekano wa upotevu wa dawa na vifaatiba pasipo uongozi kuwa na taarifa. Menejimenti inashauriwa kuchunguza jambo hili ili kubaini kama kweli bidhaa hizo bado zipo safarini,” inasema taarifa ya CAG.


Msimamo wa Muhimbili
Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema MNH inazo hati za kupokelea ‘Develivery note’ za mizigo iliyopokea bila ankara, kinachohitajika ni MSD kuoanisha ankara walizozitaja na hati walizozifikisha hospitalini hapo.

Aligaesha alisema namba za ankara zilipatikana kwenye maelezo ya MSD yaliyowasilishwa MNH ikionyesha matumizi ya hospitali kwenye akaunti iliyopo MSD kutokana na fedha ambazo Serikali inapeleka huko.


“Ili kukamilisha utaratibu wa kupeleka mzigo mahali, mzigo huo unapaswa uambatane na nyaraka kama mkataba kati ya mnunuaji na muuzaji, ankara na hati ya kupokelea. Endapo mzigo ulioletwa ni wa msaada, mkataba hauhitajiki, kwenye msaada ni lazima hati ya kupokelea iwepo na nakala inayoonyesha thamani ya mzigo,” alisema.


Alisema kwa muda mrefu imekuwa ni kawaida MSD kupeleka baadhi ya mizigo Muhimbili au wazabuni walioagizwa na MSD ikiwa haina viambatanisho hivyo muhimu, kwani mpaka sasa Muhimbili ina orodha ya mali ambazo zilipelekwa kwa kutumia hati ya kupokelea katika kipindi husika.


“Hata hivyo, tulifuatilia ankara za mizigo iliyokwishapokewa kutoka MSD ili tuweze kupewa ankara husika kwa mizigo tuliyopokea bila kiambatanisho hicho, lakini kwa bahati mbaya ankara zilizodurufiwa kutoka kwenye mfumo wa MSD hazionyeshi namba ya hati (customer reference) na hazijasainiwa na wao wala sisi,” alisema Aligaesha.


Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (kulia), akizungumza katika mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Victoria Elangwa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Sako Mwakalobo.

Ofisa Uhusiano Mkuu wa MSD, Etty Kusiluka (kulia), akizungumza katika mkutano huo wakati akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa MSD (kushoto), kuzungumza na wanahabari.Katikati ni Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Shughuli za Kanda, Terry Edward.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post