Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Amruka Anne Kilango,Ashangaa Alipewa na Nani Taarifa Kuwa Wilaya Yake Haina Watumishi HewaWakuu wa wilaya za mkoa wa Shinyanga ,kulia ni Hawa Ngh'umbi kutoka wilaya ya Kishapu,katikati mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro,kushoto ni Vita Kawawa kutoka wilaya ya Kahama-Picha kutoka Maktaba ya Malunde1 blog


Siku moja baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango kuvuliwa uongozi kwa kutosema ukweli, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ng’humbi ameiruka taarifa ya kutokuwapo kwa watumishi hewa, ambayo amesema ilimshtua alipoiona kwenye televisheni.


Mkoa wa Shinyanga unaundwa na wilaya tatu ambazo ni Shinyanga, Kishapu na Kahama zinazoundwa na halmashauri sita ambazo ni Kishapu, Manispaa ya Shinyanga, Mji wa Kahama, Ushetu, Msalala na Shinyanga Vijijini.


Rais John Magufuli juzi alitengua uteuzi wa Kilango, ikiwa ni siku 30 tangu alipotangaza kumteua kwa maelezo kuwa alitoa taarifa isiyo ya kweli kuwa Shinyanga hakuna watumishi hewa kabla ya kujiridhisha.


Pamoja na Kilango, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Shinyanga, Abdul Dachi, kwa sababu hiyo ya kutoa taarifa za uongo.


Dk Magufuli alichukua uamuzi huo baada ya kutuma timu mkoani Shinyanga kufanya uhakiki na kubaini kuwa kulikuwa na watumishi hewa 45 katika wilaya moja ya Shinyanga kabla ya kwenda wilaya nyingine za Kahama na Kishapu.


Akizungumzia sakata hilo jana baada ya uamuzi wa Dk Magufuli, Ng’humbi alisema taarifa za kukosekana watumishi hewa kwenye wilaya yake alizisikia kwenye taarifa ya habari ya televisheni Machi 30 na zilimshtua.


“Binafsi nilishtuka sana nilipoona ikitangazwa kuwa mkoa mzima wa Shinyanga, hakuna mfanyakazi hewa wakati mimi sikuwa hata nimeona taarifa kutoka wilayani kwangu iliyoandaliwa na uongozi wa halmashauri,” alisema Ng’humbi.


“Nilijiuliza taarifa imefikaje kwa mkuu wa mkoa bila kupitia kwangu? Kusema kweli nilianza kuifanyia kazi taarifa hiyo na ninatarajia ifikapo Ijumaa nitakamilisha kazi hiyo.”


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Alphonce Gagambobyaki alisema hadi sasa ofisi yake haijafahamu nani aliyempa mkuu wa mkoa taarifa ya ukaguzi wa wafanyakazi hewa kwa sababu taarifa aliyonayo mezani haijasainiwa.


“Kuna tatizo la ofisi hii kukaimiwa na zaidi ya watu wanne tangu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Dalikunda Kimulika alipostaafu Februari. Ni vigumu kujua nani alihusika nayo bila kuona saini,” alisema Bagambobyaki.

Alisema taarifa hiyo inaonekana haikusainiwa kutokana na hofu baada ya watumishi waliobainika kutokuwapo kwenye vituo vyao vya kazi karibu wote kuonekana kuwa na ruhusa maalumu.


“Wakati bado tunajiridhisha kujua ni ruhusa ya aina gani na hawa watumishi wako wapi, ndipo taarifa ilipotangazwa kwamba mkoa hauna watumishi hewa,” alisema.

Hata hivyo, alisema anaamini taarifa sahihi itajulikana baada ya timu maalumu iliyotoka Tamisemi kukamilisha uhakiki wilayani humo jana.


“Timu ile ya Tamisemi imekwenda mbele zaidi katika uhakiki wake kwa kukagua mtumishi mmoja mmoja hadi vijijini na imekamilisha kazi yake jana,” alisema Bagambobyaki.

Kuhusu iwapo aliyekuwa mkuu wa mkoa alitumia taarifa zao au la? kaimu mkurugenzi huyo alisema: “Iwapo RC alitumia taarifa zetu au la, hilo siwezi kulisemea kwa sasa.”


Kilango ambaye juzi alisema hakuwa amepata taarifa hivyo asingeweza kuzungumzia kutenguliwa kwake, jana alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kabisa na Dachi akaeleza kuwa ameupokea uamuzi huo kwa kuwa Rais ndiye mteule wake.


Taarifa ya kutenguliwa kwa watumishi hao wa umma sasa imekuwa kaa la moto kwa wakuu wa wilaya makatibu tawala wao, na wakurugenzi watendaji wa halmashauri za mkoa huo.


Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo za watumishi hewa, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alisema hawezi kuzungumzia lolote.


“Sisemi lolote na wala sizungumziii mkoa,” alisema na kukata simu ambayo haikupokewa tena.

Kama ilivyokuwa kwa mkuu wake wa wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Shinyanga, Lewis Kalinjuna aligoma kuzungumzia uwezekano wa halmashauri yake kutoa taarifa zilizompotosha Kilango.


“Sitaki kulizungumzia hilo, nawaachia wanaolijua walizungumzie,” alisema Kalinjuna.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa alikata simu yake mara kadhaa alipopigiwa na baadaye kutuma ujumbe mfupi wa maneno akisema yuko kwenye kikao na kuelekeza atumiwe ujumbe ambao hata alipotumiwa hakujibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post