Mahakama ya Kisutu DSM Yaondoa Shtaka La 4 La Utakasaji wa Fedha Dhidi ya Harry Kitilya na Wenzake Wawili


Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeliondoa shtaka la nane la utakatishaji fedha dhidi ya kamishna mkuu wa zamani wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake na kufanya idadi ya mashtaka yanayowakabili kubaki saba ikiwamo ya hati ya mapendekezo ya uwezeshwaji wa mkopo na kujipatia dola za Marekani milioni 6 mali ya serikali.
 

Hatua hiyo imefikiwa mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Emmilius Mchauru baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili mapema Aprili 8, mwaka huu. 
 

Mahakama imeona utetezi wana hoja ya msingi na kwamba kifungu cha 12 A cha mwenendo wa makosa ya jinai kilichotumika kufungua shtaka hilo kina mapungu kisheria. 
 
 

Hakimu akasema kifungu hicho kinataka kwamba kila kinapotumika kwenye makosa yake yawe ya kujitegemea kisheria.
Hata hivyo baada ya uamuzi huo, upande wa utetezi ukiongozwa na jopo la mawakili wanne, Dk. Ringo Tenga, Majura Magafu, Alex Mgongolwa na God Nyaisa uliomba mahakama kuwasilisha maombi mapya. 
 

Magafu alidai shtaka la kwanza hadi la saba, kwa mujibu wa kifungu cha 148 kidogo cha kwanza (1) na 193 A (1), washtakiwa ni watanzania wana wadhamini wa kuaminika wakipata dhamana watafuata masharti yatakayowekwa na mahakama. 
 

Hata hivyo mahakma iliahirishwa kwa muda wa dakika 20 na baada ya muda wakili wa serikali mkuu, Osward Tibabyekomya aliwasilisha pingamizi jipya kwamba mahakama hiyo haitakiwi kuendelea kufanya chochote katika kesi hiyo kwa kuwa upande wa jamhuri umewasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa kuliondoa shtaka la utakatishaji fedha haramu. 
 

Tibabyekomya alidai kuwa upande wa jamhuri tayari umewasilisha kusudio chini ya kifungu cha 379 kidogo cha (1) aya ya A cha CPA kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2008, kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendelea na hatua yoyote hadi rufaa itakapomalizika. 
 

Akijibu hoja za jamhuri Magafu alikiri kupokea nakala ya kusudio la kukata rufaa mahakama kuu Tanzania, kanda ya Dar es Salaam, lakini hakuna sheria inayoruhusu kuingilia hukumu ama uamuzi wa mahakama kutolewa. 
 

Alidai kuwa hoja za jamhuri hazina mashiko na kwamba wana nia ya kuwanyima haki wateja wao wasipate dhamana ambayo ni haki yao kisheria. 
 

Hakimu Mchauru alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili mahakama itatoa uamuzi wa wake Aprili 28 na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu. 
 

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine ni, wafanyakazi wa benki ya Stanbic Tanzania aliyekuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na mwanasheria wa benki hiyo Sioi Solomon.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527