KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA GEITA YATOA TAMKO ZITO KUHUSU MWANDISHI WA HABARI KUWEKWA MAHABUSU KWA AMRI YA DC
TAARIFA KWA UMMA/TAMKO  LA GPC KULAANI TUKIO LA MWANDISHI WA HABARI BARAKA TILUZILAMSOMI RWESIGA.

Chama Cha Waandishi wa habari mkoa wa Geita (GPC) Kinapenda kutoa taarifa ya kulaani vikali tukio la udhalilishaji na ukatili aliofanyiwa mwandishi wa Radio Free Africa (RFA) na Gazeti la Mwananchi wilaya ya Chato,Baraka Tiluziramsomi Rwesiga,kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Chato,Shaaban Ntarambe.

Pia,mwandishi huyo leo hii amepandishwa mahakamani mahakama ya wilaya ya Chato.


Kwamba mwandishi huyo alikwenda hospitali ya wilaya ya Chato aprili 6 mwaka huu majira ya saa 5 mchana kwa lengo la kupata ushauri wa kitabibu kama wagonjwa wengine.


Na hata kama angelikwenda kwa dhumuni la kutekeleza majukumu yake ya kiuandishi hospitalini hapo, mganga mkuu wa hospitali hiyo hakuwa na jukumu la kumfukuza kama mbwa na kumdhalilisha mbele ya kadamnasi ya wagonjwa badala yake angepaswa kuwasiliana na walinzi waliosikiliza maelezo yake na kumruhusu kuingia ndani.


Kitendo cha Daktari huyo kuacha majukumu yake ya kuwahudumia wagonjwa na kugeukia kazi ya ulinzi sisi tunaamini alipotoka na kwamba mamlaka zinazohusika zinapaswa kumpa onyo kali.


Kadhalika mbali na kitendo cha kufanya ubaguzi kwa wagonjwa kutokana na kazi wanazofanya,Geita Press Club tunaona kitendo hicho hakiendani na maadili ya utumishi wa Umma.


Tunamwomba mkuu huyo wa wilaya kutambua kuwa eneo la hospitali siyo gereza ambalo hata mwandishi akitaka kutekeleza majukumu yake lazima apate kibali.


Sisi Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita tunaamini kitendo cha mkuu wa wilaya kuamuru kukamatwa mwandishi huyo ni kutaka kuminya uhuru wa kupata habari ambao umeainishwa kikatiba na kwamba hatua hiyo inadhihilisha kuwa kiongozi huyo alikuwa na nia ovu ya kuficha mambo anayohisi ni mabaya kwake iwapo yatajulikana.


Ikumbukwe kwamba kiongozi msafi na mwadilifu hawezi kuwa na hofu na mashaka katika kutekeleza majukumu yake hata wanapofika waandishi wa habari kwake hujivunia na kuwaona kama ndugu na rafiki zake.

Kipekee tunampongeza sana Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Mponjol Latson Mwabulambo kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa viongozi wa GPC waliofika ofisini kwake ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo na kueleza ukweli kwamba polisi walitekeleza amri waliopewa na mkuu wa wilaya ya Chato kumkamata mwandishi huyo.


Msimamo wetu Geita Press Club tunamtaka Mkuu wa wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe,kumwomba radhi mwandishi huyo kwa muda usiozidi siku saba.


Kuondoa zuio la waandishi wa habari mkoani hapa kuingia hospitalini hapo kwa kibali chake.


Iwapo mambo hayo hayatatekelezwa Klabu yetu itatangaza rasmi mgogoro na uongozi wa wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kususia kuandika habari zake njema kwa maendeleo ya wilaya ya Chato.

Limetolewa na Salum Maige

KATIBU MKUU GPC

KNY. Daniel Limbe

MWENYEKITI WA KLABU YA WAANDISHI MKOA WA GEITA


 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post