Kikwete Afunguka...Asema anajiandaa Kumuachia Chama Rais Magufuli Ili Yeye Abaki Mzee Mashuhuri


Ikiwa ni takriban miezi mitano tangu kutoka madarakani, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema kwa sasa anafurahia maisha ya uhuru baada ya kustaafu kwake na kwamba anajiandaa kuwa mzee mashuhuri nchini atakapokabidhi chama.


Kikwete alistaafu rasmi Novemba 5, mwaka jana baada ya kuapishwa kwa Rais wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa Uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Juni, mwaka huu.


Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Kikwete alisema maisha nje ya Ikulu ya Magogoni, ni mazuri kwa sababu ametua mzigo wa kuhudumia watu milioni 50 na kwamba sasa anaendelea na mambo yake binafsi.


“Maisha baada ya kutoka madarakani, ni mazuri kwa sababu sina presha niliyokuwa nayo, nilikuwa na mzigo mkubwa wa kuangalia taifa hili la watu milioni 50, siyo mzigo mdogo, ni kazi kubwa, una hili, una hili unarudi nyumbani…


“Sasa hivi unarudi nyumbani hauna faili, ninafanya mambo ninayoyapanga mimi, na shughuli ninazofanya ni za kimataifa tu, niko kwenye hili la Libya (mjumbe wa usuluhishi wa mgogoro wa Libya), naondoka karibuni, tuna mkutano Marekani wa mambo ya malaria.


“Nipo kwenye Kamisheni ya Elimu na Waziri mkuu Gordon Brown, (Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza), pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nafanya shughuli nyingi tu sasa hivi," alisema na kuongeza:


“Kuhusu siasa, bado ni Mwenyekiti wa CCM na baada ya muda, nitakabidhi (chama) baada ya hapo kila kitu nitamuachia mzee Magufuli aendelee nayo, mimi nitabaki ni mzee tu maarufu katika nchi yetu, maisha ni mazuri tu."


Novemba, mwaka jana, baada ya kutoka madarakani, Kikwete kwa mara ya kwanza alionekana eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam alipokwenda kufanya manunuzi na mkewe Salma.


Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa Kikwete alikuwa amevalia suti maarufu kama ‘kaunda suti’ ya rangi nyeusi, alionekana akiingia katika viunga vya Mlimani City saa 5:00 asubuhi.


Mashuhuda wa tukio hilo, walisema Kikwete aliwasili katika maeneo hayo akiwa katika msafara wa magari manne na pikipiki moja.


Hatua hiyo ilionekana kushangaza baadhi ya watu waliokuwapo katika maeneo hayo, huku wengi wao wakionekana kutaka kumsalimia.


Akiwa kwenye eneo hilo, Kikwete na mkewe, waliingia katika maduka ya Game na kufanya manunuzi kwa dakika zisizopungua 10 hadi 15 na baadaye kutoka nje na walinzi wake wakionekana kubeba mifuko iliyokuwa na bidhaa walizonunua.


Kama ilivyo hulka ya Rais Kikwete, alipotoka nje ya duka hilo, alianza kusalimiana na mtu mmoja ambaye alionekana kufahamiana naye.


Hatua hiyo ilimpa fursa ya kuwasalimia watu wengine waliokuwa karibu na tawi la benki moja.


Baada ya hapo, msafara wake uliondoka na kuelekea barabara ya Sam Nujoma.


Tangu achaguliwe kuwa Rais mwaka 2005, itifaki na majukumu yake ya urais, yalikuwa yakimbana Rais Kikwete na hivyo kushindwa mambo yake binafsi kama walivyo raia wengine.


Aidha, tangu alipoachia kiti cha urais na kumkabidhi Dk. Magufuli baada ya kuapishwa Novemba 5, mwaka jana, Kikwete amekuwa akiishi nyumbani kwake Msoga mkoani Pwani na mara chache amekuwa akienda Ikulu kuteta na Rais Magufuli.


Kikwete aliondoka rasmi Ikulu na familia yake Novemba 6, mwaka jana na kuanza maisha mapya kijijini kwake Msoga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post