Hospitali ya Muhimbili Wachanganya Maiti,Ndugu Wasafirisha na Kuzika Maiti Isiyo Yao

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeingia katika mkasa baada ya kutoa mwili wa marehemu kwa watu tofauti ambao nao bila ya kujua, waliusafirisha na kuuzika Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Kutokana na kosa hilo, hospitali hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, jana walilazimika kufukua maiti hiyo ya Janeth Bambalawe (65), kuirejesha Dar es Salaam ili ikabidhiwe kwa wahusika baada ya kusafirisha maiti ya Amina Msangi (79), ambayo iliachwa kwa makosa katika chumba cha kuhifadhia maiti hadi Usangi.

Ilivyokuwa

Sintofahamu hiyo ilitokea juzi asubuhi baada ya ndugu wa Janeth, kufika mochwari Muhimbili ili kuuchukua mwili wa marehemu huyo kwa ajili ya maziko katika makaburi ya Kipunguni, Ukonga na kuukosa.

Akizungumzia mkasao Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi MNH, Dk Praxeda Ogweyo alisema ndugu wa Amina ambaye alifariki Aprili 8 hawakuukagua mwili wa marehemu baada ya kupewa na badala yake waliondoka na mwili wa Janeth.

Alisema marehemu Amina aliyefikishwa hospitalini hapo kwa rufaa akitokea Temeke Aprili 6 na kulazwa wodi 12 katika jengo la Kibasila, alihifadhiwa jokofu moja na Janeth ambaye alifikishwa hapo kutokea Amana Aprili 4 na kulazwa wodi 2 jengo la Mwaisela. Naye pia alifariki Aprili 8.


“Wote walifariki siku moja, wakahifadhiwa katika jokofu moja kwa hiyo mtumishi wa mochwari alipokwenda kuutoa mwili alichanganya badala ya kuwapatia mwili wa Amina, akawapa ule wa Janet na ndugu nao hawakushiriki kikamilifu kukagua,” alisema Dk Ogweyo.
Alisema kwa kutambua kosa hilo, Muhimbili ilitoa gari la wagonjwa na wafanyakazi wawili kwa ajili ya kuupeleka mwili wa Amina, Usangi kwa ajili ya mazishi na kuurejesh Dar es Salaam ule wa Janeth. Pia iliwasiliana na jeshi la polisi kwa ajili ya taratibu za kufukua mwili huo. “Wawakilishi wetu wamekwenda Mahakama ya Mwanzo, Wilaya ya Mwanga kwa ajili ya viapo na baadaye jioni watafukua mwili tayari kwa safari ya kuurejesha kwa ndugu husika kwa mazishi,” alisema.

Alipopigiwa baadaye jioni Dk Ogweyo alisema: “Mwili unafukuliwa sasa na baada ya kukamilisha, watauandaa na wataanza safari usiku (jana) kuurudisha Dar es Salaam, tunatarajia watafika alfajiri au asubuhi (leo).”

Mbali na hatua hiyo, Dk Ogweyo alisema mtumishi aliyefanya kosa hilo amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Akielezea hali ilivyokuwa mtoto wa marehemu Janeth, Peter Mkude alisema walipofika Muhimbili aliingia na kuonyeshwa mwili wa mama yake ambao hakuutambua, akatoka na aliporudi mara ya pili aliongozana na mama zake wadogo wawili na dada yake, lakini pia hawakuutambua.

Kuona hivyo walikwenda katika ofisi za utawala ambako waliongozwa kwa mwanasheria ambaye baada ya maelezo, waliongozana naye hadi mochwari na baada ya kuthibitisha kwamba mwili umekosekana, walikwenda Kituo Kikuu cha Polisi ambako waliandikisha maelezo na kupewa ahadi ya kurejeshewa mwili wa ndugu yao.

“Walituambia kwamba wataufukua na kufikia Aprili 13 (leo) tutakuwa tumeupata, tumepanga kuzika siku hiyohiyo katika makaburi ya Kipunguni Mashariki, Ukonga saa 10 jioni,” alisema Mkude.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post