Hawa Ndiyo WEZI 13 Wajinga Zaidi Duniani




Chojnowski alilala baada ya kutekeleza wizi

Katika karibu kila jambo duniani, mwanadamu huhitajika kutumia akili ili kufanikiwa. Bila shaka, iwapo utatarajia wazidi watu wengine hasa katika kuwapora au kuwaibia basi utahitajika kuwa na ujanja zaidi. Lakini maeneo mbalimbali duniani kunao wahalifu ambao walionekana kupungukiwa.

Majuzi kwa mfano, wanaume wawili kutoka Skegness, Lincolnshire, walijipiga picha wakiimba pesa kutoka kwenye mitambo ya kucheza Kamari Bradford, Uingereza. Hawakuenda mbali, kwani walikamatwa muda mfupi baadaye Benjamin Robinson, 30, alifungwa jela miezi 32, naye Daniel Hutchinson akahukumiwa kifungo cha miezi sita jela ambacho kimeahirishwa.

Hawako peke yao. Hapa ni msururu wa wahalifu wengine waliojichongea:
1. Jambazi aliyejitapa Facebook

Andrew Hennells alikamatwa baada yake kuandika kwenye Facebook akijisifu kuhusu mpango wake wa kushambulia duka la jumla la Tesco eneo la King's Lynn, Norfolk.



Andrew Hennells aliweka picha yake na ya kisu Facebook

Aliweka kwenye Facebook picha yake ya kujipiga yaani ‘selfie’, picha ya kisu na kuandika: "Doing. Tesco. Over." (Nafanya. Tesco. Twende).

Alikamatwa na polisi dakika 15 baadaye akiwa na kisu chake na pesa £410 alizoiba. Alifungwa jela miaka minne Aprili mwaka jana.
2. Mwizi aliyetekwa na usingizi

Wachumba katika eneo la Lancashire walirejea kutoka likizoni mwaka 2014 na kumpata mwizi amelala usingizi wa pono katika kitanda chao.


Chojnowski alilala kitandani baada ya kufua nguo zake za ndani

Martin Holtby and Pat Dyson walishangaa kumpata mwizi huyo Lukasz Chojnowski, alikuwa ameosha vyombo, akafua nguo zake za ndani na hata kununua mboga.

Wanasema nyumba yao haikuwa safi sana walipoondoka kwenda likizoni. Walipata Chojnowski, aliyetoka Poland lakini akahamia Leeds, alikuwa amefanya usafi vilivyo.

Chojnowski, 28, alikiri kosa la kuvunja nyumba na akatakiwa kukaa miaka miwili bila kutenda kosa na kulipa gharama ya £200.
3. Wezi wa penguini

Watalii wawili kutoka Wales walijipata taabani 2012 baada yao kulewa na kuiba ndege aina ya penguini kwa jina Dirk kutoka kituo cha Sea World, Australia.

Rhys Owen Jones, 21, na Keri Mules, 20, waliamka baada ya ulevi kuisha na wakajipata na ndege huyo katika chumba chao. Walijaribu sana kumlisha na kumtunza kwa kumuweka kwenye bafu, mahakama iliambiwa.

Baadaye walimwachilia kwenye mtaro. Walionekana na majirani ambao waliwapasha habari polisi na wakakamatwa. Hakimu aliwatoza dola 1,000 za Australia (kiasi sawa na £637) kila mmoja na kuwashauri wasiwe wanakunywa vodka sana. Dirk alirejeshwa Sea World akiwa salama.
4. Mwizi aliyewatumia polisi picha nzuri

Mwanamume aliyekuwa akisakwa kwa makosa ya kuteketeza na kuharibu mali alituma picha ya selfie kwa maafisa wa polisi akisema picha iliyotumiwa na maafisa hao katika tangazo la kutafutwa kwake haikuwa ya kupendeza.


Picha ya kushoto ndiyo iliyokuwa imetumiwa na polisi. Aliwatumia iliyo kulia

Donald "Chip" Pugh aliwatumia maafisa wa polisi picha aliyojipiga mwenyewe na kuandika ujumbe unaosema: "Hii hapa picha yangu nzuri, hiyo mliyotumia ni mbaya sana”.

Polise katika mji wa Lima, jimbo la Ohio, walikuwa wamepakia picha kwenye ukurasa wao wa Facebook wakiomba msaada wa kumtafuta Bw Pugh.

Polisi walimjibu na kusema angefanya hisani zaidi kwa kujifikisha kwao.

Alikamatwa baadaye jimbo la Florida.

Soma zaidi hapa: Mshukiwa anayesakwa atumia polisi 'selfie'
5. Gaidi aliyejitokeza kudai zawadi

Maafisa nchini Afghanisan waliachwa vinywa wazi baada ya kamanda mmoja wa kundi la Taliban kujisalimisha na kisha kujaribu kudai zawadi ya $100 iliyokuwa imeahidiwa mtu ambaye andesaidia kukamatwa kwake.

Mohammad Ashan, alituhumiwa kupanga mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Marekani na Afghanistan mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti zinasema alifika katika kizuizi cha polisi mwaka 2012, akaelekeza mkono wake kwenye bango lenye picha yake na kisha akadai zawadi hiyo ya $100.

Maafisa wa usalama walishangaa sana na kushindwa kuelezea kitendo chake. Afisa mmoja wa Marekani anadaiwa kuambia wanahabari: “Kusema kweli, mwanamume huyu ni mpumbavu.”
6. Aliyetishia watu kwa tango

Mwanamume mmoja alijaribu kuwaibia wacheza bahati nasibu Glasgow kwa kuwatishia akiwanyooshea tango, kwa Kiingereza cucumber.

Gary Rough aliwanyooshea tango hilo likiwa limefunikwa kwa soksi na kudai pesa kutoka kwa mwanamke aliyekuwa kwenye kaunta eneo la Ladbrokes, Shettleston nchini Uingereza.

Alikabiliwa na kukamatwa na polisi ambaye hakuwa kwenye zamu.

Awali, aliambia polisi alikuwa akifanya mzaha, na kisha akawauliza: „Nitaenda jela kwa sababu ya hili?”Alifungwa jela na Mahakama Kuu ya Glasgow 2014 baada ya kukiri kosa la kushambulia watu akiwa na lengo la kuwaibia.
7. Mwanamume aliyewatania polisi Facebook

Mhalifu mtoro alijidhani alikuwa mjanja sana na akashawishika kuwacheza polisi wa Gwent, Uingereza waliokuwa wamepakia ujumbe kwenye Facebook wakiomba usaidizi kutoka kwa umma kumkamata Februari mwaka jana.

Logan James, aliyekuwa na umri wa miaka 19 alikuwa akitafutwa kwa kukiuka masharti ya kuachiliwa kwake jela. Kijana huyo kutoka Caerphilly alikuwa awali amefungwa kwa kuwajerushi na kuwashambulia watu na pia kuwa na kisu.

"Haha nishikeni iwapo mnaweza, hamtajua nikiponyoka,” aliwacheka. Baadaye aliambia shirika la habari: “Nimekuwa nikitembea karibu na nyumbani kwangu kwa hivyo hawajatia bidii kunikamata.”


Alikamatwa baadaye siku hiyo. Polisi walimshukuru kwa kuwasaidia kumkamata.
8. Mwizi aliyeshindwa kufungua mlango

Mwizi mwingine James Allan alinaswa kwenye kamera ya CCTV akitekeleza wizi katika duka moja Abingdon, Oxfordshire mwaka 2012.

Ingawa hakutaka kuonekana uso wake, aliangukia mtambo wa kuhifadhi vinywaji na mwishowe akalazimika kuivua barakoa yake kutoka kichwani.

Alijaribu kufungua mlango atoroke lakini akashindwa kwani badala ya kuuvuta mlango, alikuwa anausukuma.

Mwanamke ambaye mwizi huyo alikuwa amemzuilia akitumia bunduki bandia ndiye aliyemsaidia kuufungua mlango huo.

Isitoshe, Allan aliyekuwa na umri wa miaka 29 wakati huyo, alikuwa amejaribu kuiba kutoka kwenye duka hilo siku 10 awali.

Alifungwa jela miaka mitatu kwa kosa la wizi, miaka miwili kwa kuwa na silaha au mwigo wa silaha. Vifungo hivyo alitakiwa avitumikie sambamba.
9. Mwanamume aliyetumia mfuko kujifunika

Mwizi mmoja Christopher Badman, kutoka Bridgend kusini mwa Wales, alitumia mfuko wa kubebea bidhaa kuficha kichwa chake alipokuwa akitekeleza wizi katika hoteli moja Porthcawl wakati wa mkutano wa kumkumbuka Elvis Presley.

Alishawishika kutoa mfuko huo kichwani alipokuwa ameangalia kamera ya CCTV.

Polisi walimtambua kwa urahisi na kumkamata.

Badman alikiri kuvunja na kuingia kwenye hoteli hiyo na akatakiwa kulipa £900 kama na £100 juu.
10. Jambazi akwama dirishani

Mwizi mmoja nchini Uchina alihitaji kusaidiwa na watu baada yake kukwama kwenye dirisha nyembamba akijaribu kuingia kwenye nyumba moja ghorofa ya tano.

Alishindwa na kubaki amening’inia.

Iliwachukua waokoaji dakika 30 kumuokoa.

Alikabidhiwa kwa maafisa wa polisi.
11. Mwizi wa benki aliyeacha anwani yake

Mwizi wa benki aliyejaribu kujificha kwa kuvalia miwani ya giza n ahata kuvalia soksi juu ya viatu vyake, alisahau kwamba alikuwa ameacha anwani yake.

Dean Smith, 27, alikuwa ameenda kwenye tawi la benki ya Barclays eneo la Treorchy, Wales kubadilisha anwani yake alipovutiwa na pesa zilizokuwa kwenye meza.


Smith baadaye alikiri kwamba alikuwa "mjinga sana"

Alirejea baadaye akiwa amevalia miwani hiyo ya giza na soksi na kumtaka keshia ampe pesa hizo. Keshia alikataa na akalazimika kutoroka mikono mitupu. Polisi walimpata kwa njia rahisi baada ya kufuatilia video ya kamera ya CCTV, wakamtambua na kisha kufahamu anwani yake.

Alikiri kwamba alikuwa “mjinga sana”. Alifungwa miaka miwili unusu.
12. Mwizi wa gari azimwa na auto-lock

Mwizi wa gari katika mji wa Pretoria, Afrika Kusini, alizimwa baada ya mfumo wa kufunga gari wa auto-lock kulifunga gari baada yake kuingia ndani.

Alikwama kwa saa moja unusu akiitisha usaidizi. Wapita njia walimcheka tu hadi mwenye gari aliporejea, akiwa ameandamana na polisi, kwa mujibu wa gazeti la The Star.

"Unafanya nini ndani ya gari langu?” alimwuliza mwenye gari kabla ya kumfungulia, na polisi walioandamana naye wakamkamata mara moja.
13. Simu ilivyomponza mwizi

Wezi wengi wamekamatwa kutokana na picha za kujipiga, yaani selfie, na Ashley Keast, bila shaka hatakuwa wa mwisho. Alitumia laini ya simu aliyokuwa ameiba kujipiga picha akiwa ndani ya nyumba ambayo alikuwa amevunja na kuingia 2014

Mwanamume huyo kutoka Rotherham baadaye alipakia picha hiyo kwenye Whatsapp lakini bila kujua akamtumia mfanyakazi mwenzake mwenye nyumba aliyokuwa amevunja.

Maafisa wa polisi walimpata kwake nyumbani akiwa na saa aina ya Rolex ya thamani ya £4,000 aliyokuwa ameimba.

Keast, aliyekuwa na umri wa miaka 25 wakati huo, alifungwa jela miaka miwili na miezi minane baada ya kukiri kosa la kuvunja nyumba na kutekeleza wizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post