Askofu Gwajima: Mafisadi Ndiyo Wanaona Uongozi wa Rais Magufuli Haufai



Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema mafisadi walioinyonya nchi katika Serikali ya awamu ya nne, ndiyo wanaoona utawala wa Rais John Magufuli haufai.



Akizungumza masuala ya kitaifa kwa kifupi, huku akitoa mafundisho kwa waumini wake jana katika ibada kanisani kwake, Gwajima alimtaka Dk Magufuli aendelee kushikilia uzi huo huo bila kuulegeza. 




Gwajima ambaye mwaka jana, wakati wa vuguvugu za kampeni ya Uchaguzi Mkuu, aliwahi kusema wasiopenda kuona yeye akimsaidia aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa basi wachukue ndimu wale, jana alisema mafisadi ni wachache na Magufuli anafanya kazi ili kuhakikisha Watanzania wengi wananufaika na uongozi wake. 




Mara kadhaa, Askofu Gwajima alikaririwa akisema kuwa atamsaidia kiongozi yeyote mwenye lengo la kuleta mabadiliko ya taifa, bila kujali anatoka chama gani. 




Katika mikutano yake, Gwajima alikuwa akiwataka waumini wake kuchagua kiongozi wanayedhani atawaletea mabadiliko, na alikaririwa na vyombo vya habari akiingia katika malumbano makali na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa ambaye mbele ya waumini wake alimwita kuwa ni rafiki yake. 




Jana akimzungumzia zaidi Dk Magufuli, Askofu Gwajima alisema, “wasikukatishe tamaa endelea hivyo hivyo kuna wanyonyaji walipenyeza mirija yao katika Serikali iliyopita wakati wao umefika, wanatapatapa.” 




Askofu Gwajima alisema yeye ataendelea kupambana na ufisadi kumsaidia Dk Magufuli kwa kutumia jina la Yesu Kristo na si vyombo vya dola. 




Alisema mkono wake ni mgumu kama wa chuma na kwamba kwa kulitumia jina hilo, hawezi kushindwa kuwashughulikia watu wa aina hiyo. 




“Nitatumia jukwaa hili hili la Yesu Kristo kuwasambaratisha wasioitakia mema Serikali ya Magufuli, kwani zama zao zimekwisha,” alisema. 




Askofu huyo alisema kuna taasisi zilifikia hatua ya kutengeneza magonjwa na hizo hizo zinatoa misaada ya dawa kwa Tanzania.


“Yaani makampuni yanatengeneza magonjwa halafu hao hao wanatoa misaada ya dawa hizo kwa Tanzania, unajiuliza ilikuwa serikali ya namna gani,” alisema. 




Alisema taasisi hizo ziko tayari kuua Watanzania ili kujipatia fedha chafu ambazo maisha ya ndugu zetu yanapotea. 




“Kuna watu wananiuliza Gwajima Ufufuo na Uzima ni kanisa, dhehebu au wanaharakati unasema kila kasoro iliyo mbele yako, nikawajibu ni majeshi ya Yesu Kristo,” alisema. 




Aliyataka madhehebu mengine ya dini kukemea maovu ili kuleta maisha bora ya waumini wao. 




Gwajima aliwataka waumini hao, kutumia jina la Yesu Kristo kila wanafanya ibada kwani maombi yao yatajibiwa kwa kutaja jina hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post