Picha !! RAIS MAGUFULI ATII AGIZO LA MKUU WA MKOA WA DAR KUHAKIKI SILAHA,ASEMA NI AIBU ASKARI POLISI KUNYANG'ANYWA SILAHA NA JAMBAZI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa mtu kwanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam la kuhakiki silaha, ambapo bunduki zake mbili aina ya Shortgun na Pistol zimehakikiwa nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar es salaam.

Uhakiki huo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa Silaha, na ametoa wito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchi nzima kuhakikisha zinahakikiwa.

Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na watu wanaojihusisha na vitendo vya uharifu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.

"Ni aibu kumuona askari polisi mwenye silaha ananyang'anywa silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang'anye silaha na wewe una silaha?" Amehoji Rais Magufuli

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuunga mkono zoezi hilo na amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea kiti cha Umeya katika Jiji la Dar es salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata Meya katika uchaguzi uliopangwa kufanyika kesho tarehe 22 Machi, 2016 badala ya kuendelea kurumbana.

Dkt. Magufuli amesema upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi huo, ili Meya apatikane na Jiji liweze kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.

"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya kweli" ameongeza Rais Magufuli

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam


Kamanda wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna CP Simon Sirro kulia akimkabidhi Silaha aina ya Bastola Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya uhakiki uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.


Kamanda wa Kanda Maalum ya Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna CP Simon Sirro kulia akimkabidhi silaha aina ya shortgun Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya uhakiki uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiiweka silaha yake vizuri mara baada ya kuhakikiwa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527