MWANAMKE ALIYEOLEWA NA WANAUME WAWILI HUKO KATAVI AFARIKI DUNIA


Wanandoa Arcado Mlele(kushoto) na Paulo Sabuni(kulia) wakiwa na mke wao  Veronica Salehe na watoto wao Fred na Wilson...enzi za uhai wake-Picha kutoka Maktaba ya Malunde1 blog
******

Mwanamke Mkazi wa Kijiji cha Ikondamoyo Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi Veronica Salehe 54 aliyekuwa amefanya uamuzi adimu wa kuolewa na wanaume wawili kwa kipindi cha miaka tisa amefariki Dunia.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikondamoyo John Maganga amesema Veronica alifariki wiki iliyopita Mkoani Tabora alikokuwa amekwenda kupatiwa matibabu kwa kaka yake.

Katika uhai wake wa ndoa iliyowezeshwa na mume mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo ilielezwa kuwa mwanamke huyo ndiyo alikuwa amewaoa wanaume hao kwa kipindi cha miaka tisa huku akiwa na amri kuu katika nyumba kama ilivyo katika ndoa za kawaida.

Wanaume hao waliokuwa wakiishi naye ni Paulo Sabuni (62) ambaye ndiye aliyekuwa mume mkubwa na Arcado Mlele (47) ambaye alikuwa ni mume mdogo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Veronica na mume mkubwa walifika kijijini hapo miaka 24 iliyopita wakiwa wametokea Kijiji cha Usumbwa mpakani mwa Chunya na Tabora na walipofika kijijini hapo walikuwa wakijishughulisha na shughuli za kilimo na biashara ya kuuza pombe ya kienyeji aina ya komoni.

Katika uhai wake Veronica alibahatika kuwa na watoto wanne wawili wa kike na wawili wa kiume ambapo mtoto ambaye ni wa mume mdogo ni wa kiume ana miaka tisa anasoma darasa la nne shule ya msingi Ikondamoyo na watoto watatu ni wa mume mkubwa .

Maganga alisema maisha yake ya kuishi na wanaume wawili haikuwa siri kijijini hapo na wanakijiji walikuwa wamewazoea kwani walikuwa wakiishi kwa amani na mume mdogo alikuwa akiishi kwenye nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake lakini alikuwa akishinda kwa mume mkubwa ambako kulijulikana hapo kijijini kuwa ni nyumba kubwa.

Basi pale mambo yote yalikuwa kula ,kunywa na mama huyo alikuwa akiwapangia zamu wanaume hao kama afanyavyo mume mwenye wake wengi na wao walikuwa wanaridhika na kufurahia maisha hayo.

Alieleza kwamba katika siku iliyokuwa mama huyo amechoka kupika mume mdogo alikuwa akichukua jukumu la kupika na kumwandalia chakula mume mkubwa na maji ya kuoga.

Pia  ilipokuwa zamu ya mama huyo kula kwa mume mkubwa alikuwa anahakikisha anamfulia nguo mume mkubwa na kisha anakwenda kwa mume mdogo naye anamfulia nguo.

Maganga alisema ndoa ya mama huyo na mume mdogo ilivunjika mwaka jana baada ya mume mdogo Arcado Mlele kuamua kuachana na mama huyo na kuamua kuondoka na mtoto wake ambaye anaishi naye Kijijini hapo.

Alieleza katika shughuli za matanga ya msiba wa marehemu Veronica wanaume hao wote wawili walishirikiana katika shughuli zote za kumaliza msiba huo zilizofanyika hivi karibuni Katika kijiji cha Ikondamoyo nyumbani kwa Sabuni Salehe.
 
Na Walter Mguluchuma -Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post