MAHAKAMA YAAMURU UCHAGUZI WA MEYA DAR KUFANYIKA LEO


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam, kufanyika leo kama ilivyopangwa.


Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema alitoa uamuzi huo jana akijibu maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na walalamikaji, Suzan Massawe na Saad Mohammed Kimji kupitia wakili wao, Elias Nawela dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.


Wakati Mahakama ikitoa uamuzi huo, Rais John Magufuli amezitaka pande zinazogombea kiti cha umeya Dar es Salaam, kukamilisha mchakato huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika leo, badala ya kuendeleza malumbano.


Rais alitoa kauli hiyo jana Ikulu wakati akihakiki silaha zake. Alisema pande zote ziwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi huo, ili meya apatikane na jiji liweze kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.


“Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, hiyo ndiyo demokrasia ya kweli,” alisema Rais Magufuli.


Akitoa uamuzi wa Mahakama uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na walalamikaji na walalamikiwa, Hakimu Lema alisema Mahakama haikuona sababu za msingi kati ya zilizowasilishwa na walalamikaji kuishawishi kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo.


“Siyo busara kuendelea na sababu ambazo hazijathibitishwa,” alisema Hakimu Lema alipokuwa akitoa uamuzi huo na kuongeza kwamba kwa kukosekana orodha inayoonyesha majina ya wapigakura, haijulikani kama waleta maombi ni miongoni mwa wapigakura au la.


Hakimu Lema alisema walalamikaji hawakuwa makini tangu awali walipofungua shauri hilo, Februari 5 kwani hawakutokea mahakamani hadi Februari 14, wakili wao Nawela alipojitokeza na kuomba nakala ili awapelekee wajibu maombi jambo linalofanya washindwe kuishawishi Mahakama kuwapa haki yoyote kwa kuwa hawakufuatilia shauri lao tangu awali.


Mapema jana mchana, wakili Nawela aliiomba Mahakama itoe zuio la kufanyika uchaguzi huo na iamuru hali ibaki kama ilivyo hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi kwa madai ya kwamba walalamikaji katika shauri hilo, hawajapewa haki yao ya kualikwa kushiriki katika uchaguzi huo.


Alidai kuwa iwapo uchaguzi huo utafanyika, basi maombi yao na kesi ya msingi yatakuwa hayana maana.


Akijibu hoja hizo, wakili Jumanne Mtinange kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, aliiomba Mahakama kuyaondoa maombi hayo kwa madai kuwa hayana msingi wowote.


Mtinange alidai hakuna uthibitisho wowote au orodha ya wapigakura kuonyesha kwamba waleta maombi wamekosekana, hivyo maombi ya kutaka hali ibaki kama ilivyo hayana uzito wowote.


Alisema maandalizi ya uchaguzi yana gharama na kwamba ni mara ya tatu umeahirishwa, hivyo kuomba uchaguzi wa leo uendelee kama kawaida.


Timu ya mawakili wa Chadema wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, Omary Msemo na John Mallya walikuwa muda wote wakifuatilia kesi hiyo mahakamani hapo.


Kwa uamuzi huo, kinyang’anyiro cha kugombea umeya sasa kimebaki kwa Isaya Mwita wa Chadema na Omary Yenga wa CCM wanaowania nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika leo katika Ukumbi wa Karimjee baada ya kuahirishwa mara tatu kwa sababu mbalimbali ikiwamo zuio batili la Mahakama kabla ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kuiagiza uchaguzi huo ufanyike kabla ya Machi 25.


Baadaye, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Sarah Yohana alitangaza na kutoa barua kwa wajumbe husika juu ya wito wa kikao cha Baraza la Madiwani kitakachokuwa na ajenda ya uchaguzi akisema wajumbe 163 watashiriki kupiga kura, kati yao 87 ni kutoka Ukawa na 76 CCM.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527