MAALIM SEIF AREJEA ZANZIBAR BAADA YA DR SHEIN KUAPISHWA KUWA RAIS,ALIKUWA MAPUMZIKONI SERENA HOTEL KWA SIKU 17Siku chache baada ya Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohamed Shein kuapishwa baada ya kushinda uchaguzi wa marudio uliosusiwa na baadhi ya vyama vya upinzani, Katibu mkuu wa chama cha wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amerejea Zanzibar.


Maalim Seif ambaye alikuwa mapumzikoni katika hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam kwa takribani siku 17, jana alirejea Zanzibar kuendelea na mapumziko yake.


Maalim Seif alilazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal ya jijini Dar es Salaam,mara baada ya kuruhusiwa March 8 mwaka huu alishauriwa na Daktari wake kupata mapumziko ya muda mrefu.


Kurejea kwa Maalim Seif visiwani humo kunazidisha shauku na kiu ya baadhi ya Wazanzibar kutaka kusikia atakachokisema kiongozi huyo wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa kwenye jamii.


Maalim Seif aliugua wakati Wazanzibar wakiwa katika maandalizi ya kurudia uchaguzi mkuu uliofanyika March 20, mwaka huu baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar( ZEC), Jecha Salim Jecha kwa madai kuwa uligubikwa na dosari nyingi.


Gharama za Hotelini
Taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari siku chache zilizopita zilidai kuwa kila siku aliyokaa kwenye hoteli hiyo, Maalim Seif alikuwa akitumia wastani wa Sh. 6,162,500.


Kutokana na takwimu hizo, hadi kufikia jana, Maalim Seif atakuwa ametumia kiasi kisichopungua sh. Milioni 92.4


Chumba alichokuwa akilala Maalim Seif katika Hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tano kinalipiwa dola za Marekani 2,500 kwa usiku mmoja.


Maalim Seif alikuwa akiishi hotelini hapo na wasaidizi wake watano, ambao wote gharama zao zinalipwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post