KUHUSU NYUMBA YA KAMISHNA WA POLISI KULIPULIWA BOMU HUKO ZANZIBAR



Nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame imeripuliwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu na watu wasiojulikana majira ya saa 5.00 usiku huko Kijichi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.


Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Ofisini kwake Makao Makuu ya Polisi Kilimani, Kamishna Hamdani amesema tukio hilo limeathiri sehemu ya paa la nyumba na dari na kujeruhi baadhi ya watu waliokuwa wamelala na kusababisha hasara kubwa.


Amesema tukio hilo linafanana na lile lililotokea tarehe 03 mwezi huu katika Maskani ya CCM Kisonge Unguja hivyo polisi inaendelea kufanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wanaofanya uhalifu huo.


Akizungumzia matukio mengine ya uhalifu na kuchoma moto nyumba, maskani na kituo cha Afya huko Pemba, alisema Jeshi la Polisi limeanza msako mkali na kuwatia mbaroni watu 31 ambao wanaendelea kuhojiwa na watakaohusika watafikishwa katika vyombo vya sheria.


Kamishna Hamdani amewatoa hofu wananchi kuhusu usalama wao na mali zao kuelekea uchaguzi wa marudio utakaofanyika tarehe 20 mwezi huu na kuwepo kwa ongezeko la askari katika maeneo mengi ya mijini na vijijini ni moja ya juhudi za kuimarisha ulinzi na kuhakikisha uchaguzi huo utakuwa salama na amani.


Ametahadharisha kuwa mtu yoyote atakayejihusisha kuanzisha vurugu au kufanya kitendo chenye ishara ya uvunjifu wa amani atapambambana na vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani ametoa wito kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba bila ya woga kwani jeshi hilo limejipanga kuimarisha ulinzi sehemu zote.
 
Na Mwashungi Tahir na miza Kona – Maelezo Zanzibar

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527