JINSI WATU WATATU WALIOLALA GESTI WALIVYOUAWA KISHA KUCHOMWA MOTO NDANI YA GESTI HUKO MBEYA


Watu watatu wamefariki dunia kwa kunyongwa na miili yao kuchomwa moto ndani ya nyumba ya wageni iliyopo Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.


Mauaji hayo yamegubikwa na utata kutokana na mazingira ya tukio hilo kuwahusisha wapangaji wa nyumba hiyo usiku wa kuamkia jana.


Mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Kyela Kati, Boniface Mtengela alisema waliouawa ni watatu kati ya watu wanne waliofika kwa pamoja saa nne usiku jana.


Alisema watu hao walikuwa wanaume watatu na mwanamke mmoja na waliouawa ni mwanamke na wanaume wawili.


Mtengela alisema wanaume wawili walijiandikisha kwa jina la Ali Hassan na mwanamke la Mariam.


“Mwanamume mmoja alipanga chumba namba 14, mwingine 105 na mwenye mke alipanga chumba namba 15.

"Waliokutwa wamekufa ni wanaume wawili wa vyumba na 14 na 105 pamoja na mwanamke huku mwanamume mwenye mke akitoroka,” alisema.


Mganga Mfawidhi wa Wilaya ya Kyela, Francis Mhagama alisema uchunguzi wa miili ya marehemu hao umebaini kuwa waliuawa kwa kunyongwa kisha kuchomwa moto baada ya kumwagiwa mafuta ya taa.


Uchunguzi katika eneo la tukio ulibaini miili yao iliungua, lakini chumba na magodoro havikuungua. Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kyela Kati, Timoth Luvanda alisema usiku wa tukio hilo hakusikika kelele zozote.


Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo wala kukamatwa kwa mmiliki wa nyumba hiyo na kuhojiwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kyela.


Mhudumu wa nyumba hiyo, Hagai Yohana alisema mgeni mmojawapo aliondoka kabla ya saa 12 alfajiri akiwa na kidumu na mfuko wa rambo.


Alisema wageni wote waliandikisha kuwa ni wafanyabiashara na hawakuwa na mizigo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post