IJUE HISTORIA FUPI YA KATIBU MKUU KIONGOZI MPYA ANAYEBEBA MIKOBA YA OMBENI SEFUE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amemteua Balozi Mhandisi John William Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi tarehe 6 Machi 2016, akichukua nafasi ya Balozi Ombeni Sefue. 
 
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Mhandisi Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal mwenye makazi yake jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi.

Vilevile, hadi uteuzi wake, Balozi Kijazi amekuwa Mkuu wa Mabalozi wa Afrika nchini India ambaye amekuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye asili ya Kiafrika nchini India.

Kabla ya kuwa balozi, Mhandisi Kijazi alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India. Kati ya mwaka 1996 hadi 2002.

Mhandisi Kijazi alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo.

Balozi Mhandisi Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.

Balozi Mhandisi John Kijazi amemuoa Fransiscar Kijazi na pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard Kijazi.

Balozi Mhandisi John Kijazi ataapishwa leo tarehe 7 Machi 2016 na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu jijini Dar es salaam.

Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,Wizara ya Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Kikanda na Kimataifa,07 Machi 2016.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post