CCM WAKOROGANA UJIO WA BALOZI MWAPACHU CCM,UVCCM WACHARUKA WATAKA WALIOMPOKEA WATIMULIWE



Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi wilayani Hai (UVCCM),Arnold Swai amepinga ya kurejea ndani ya chama hicho kwa mwanadiplomasia na mwanasiasa mkongwe nchini, Balozi Juma Mwapachu.


Balozi Mwapachu, juzi alitangaza kurejea CCM kwa madai ya kuridhishwa na utendaji wa Rais Magufuli.


Akizungumza na wanahabari jana mkoani hapa,Swai alisema kuwa chama hakipaswi kumpokea mwanasiasa huyo kwa madai kuwa ni msaliti huku akienda mbele zaidi na kutaka waliompokea wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za chama.


"Ni lazima tujiulize, hivi mwanadiplomasia huyo angekuwa tayari kurejea CCM kama mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa angeshinda urais?" alihoji na kuongeza:


"Hatuwezi kumpokea msaliti kama huyu, wakati chama kilipokuwa kwenye mapambano aliondoka tena kwa kejeli, leo chama chetu kimesimama imara chini ya mwenyekiti wetu Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ndio anarudi na wimbo uleule kwamba chama kimemlea, haikubaliki."


Alisema wakati wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,baadhi ya makada maarufu wa CCM walikisaliti chama huku wakitoa kauli za kejeli na kusababisha mpasuko ndani ya chama ambao majeraha yake hayajapona.


Mwenyekiti huyo alieleza kukerwa na kauli ya Balozi Mwapachu kwamba chama ndo kimemlea na kwamba hayo si maradhi ya kumuua mtu bali yanatibika, lakini dhambi ya usaliti haitibiki


"Nguvu kubwa iliyotumiwa na CCM kuwanadi wagombea wake ilisababishwa na wasaliti kama hawa,nawaomba viongozi wa ngazi za juu kutofumbia macho jambo hili kwani ni hatari kwa ustawi wa chama chetu." Alisema


Balozi Mwapachu alirejea CCM juzi na kupokelwa na mwenyekiti wa CCM kata ya Mikocheni jijini Dar es Salaam, Athuman Mareenda, ambaye alimkabidhi tena kadi ya uanachama wa chama hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527